NATO yaahidi kuendelea kuisaidia Ukraine
16 Aprili 2025
Marke Rutte ametoa ahadi hiyo ya NATO kuendelea kuisaidia Ukraine Jumanne alipokuwa katika mji wa bandari wa Odessa ambapo pia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Volodymyr Zelensky. Amesisitiza kuwa zaidi ya euro bilioni 20 za msaada wa kijeshi tayari zilishaahidiwa na washirika wa mfungamano huo wa kijeshi katika miezi mitatu ya mwanzoni mwa mwaka huu.
Mkuu huyo wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO amefanya ziara Ukraine siku kadhaa baada ya Urusi kuushambulia mji wa Summy kwa makombora mawili, na kusababisha vifo vya takriban watu 35 wakiwemo watoto wawili.
Katika ziara hiyo ya kushtukiza, Rutte akiwa ameambatana na Zelenskyy waliwatembelea wanajeshi waliojeruhiwa katika mzozo unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine. Aliwakabidhi wanajeshi hao tuzo maalum za kutambua mchango wao katika kuilinda Ukraine.
Soma zaidi: Rutte: Urusi inasalia kuwa tishio kubwa kwa NATO
Kwa upande wake Rais Volodymyr Zelensky wakati wa ziara ya Rutte amesema kuwa Waukraine ndiyo wenye maamuzi kuhusu maeneo ya taifa hilo. Ametumia nafasi hiyo kuwaonya wapatanishi wa Marekani katika mazungumzo na Urusi kuwa wasifanye maamuzi yasiyokubalika kuhusu maeneo ya Ukraine yaliyotekwa na Urusi.
Muda mfupi baada ya ziara hiyo maafisa katika mji huo wa Odessa wamesema shambulio la droni lililofanywa na Urusi kuulenga mji huo wa bandari limewajeruhi watu watatu.
Moto ulizuka baada ya shambulio hilo huku nyumba kadhaa na miundombinu ya kiraia ikiripotiwa kuwa imeharibiwa. Katika mji jirani wa Kherson mtu mmoja ameuwawa na wengine watatu wamejeruhiwa katika moja ya mashambulizi hayo ya Urusi dhidi ya Ukraine.
Ni wakati jeshi la anga la Ukraine likiripoti kuwa Urusi iliishambulia nchi hiyo kwa ndege 97 zisizo na rubani usiku wa kuamkia Jumatano. Taarifa ya jeshi hilo imesema lilifanikiwa kuzidungua droni 57 kati ya zilizorushwa. Droni 34 zinaripotiwa kuwa zilipoteza mwelekeo wakati sita zilizosalia hazikutolewa maelezo.
Urusi imeongeza mashambulizi ya droni katika mashambulizi yake dhidi ya Ukrainena mara nyingi imekuwa ikiyafanya nyakati za usiku ili kuipa ugumu mifumo ya ulinzi ya anga ya Kyiv kuyazuia.