NATO: Wanachama sasa kuongeza michango yao kwa asilimia 5
25 Juni 2025Washirika hao wa Muungano wa kijeshi wa NATO leo wamekubaliana kuongeza michango yao ya ulinzi kwa asilimia hizo 5 kwa ajili ya matumizi ya usalama hadi kufikia mwaka 2035, hayo yamewezekana baada ya Marekani kuweka msukumo.
Mpango huo ni mkubwa zaidi kufikiwa na jumuiya ya NATO tangu kumalizika Vita vya Baridi, huku kukiwa na wasiwasi kwamba Urusi inaweza kuzishambulia nchi wanachama wa Jumuiya hiyo katika miaka michache ijayo.
Tamko rasmi la mkutano huo wa kilele linasema "Tumeungana katika kukabiliana na vitisho na changamoto kubwa za usalama, hasa vitisho vya muda mrefu vya Urusi kwa nchi za Amerika ya Kaskazini na za barani Ulaya.
Washirika hao watachangia asilimia 3.5 ya Pato la Taifa kila mwaka kwa mahitaji ya msingi ya ulinzi, kama vile ununuzi wa silaha na kwa ajili ya wanajeshi wao, na watatoa pia nyongeza ya asilimia 1.5 itatumika kwenye gharama nyingine, ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu na ubunifu wa kiteknolojia ambao ni muhimu kwa mafanikio endelevu ya shirika lolote.Tamko hilo rasmi linasema, makubaliano hayo yatapitiwa tena ifikapo mwaka 2029.
Soma pia: Rutte: Trump amejitolea kwa ulinzi wa pande zote katika Jumuiya ya NATO
Makubaliano hayo ya kuongeza michango ya ulinzi ni ushindi mkubwa kwa Rais Donald Trump, ambaye mara kwa mara amelalamika kwamba Marekani inawabeba washirika wasio na uwiano katika bajeti ya ulinzi ya muungano huo wa kijeshi wa NATO. Hadi sasa, nchi wanachama zimekuwa zinachangia asilimia 2 tu ya Pato lao la uchumi wa Taifa kwenye ulinzi.
Mataifa 32 wanachama wa NATO, yalikabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya wanachama kama Uhispania ambayo awali ilipinga kuongeza bajeti kwa ajili ya matumizi ya ulinzi, ikisema haitaweza kulifikia lengo hilo.
Hata hivyo Uhispania hii leo imemhakikishia katibu mkuu wa NATO Mark Rutte kwamba itatimiza malengo mapya ya NATO kwa sababu imeruhusiwa kuchangia chini ya asilimia 3.5 ya Pato lake la Taifa, katika hatua inayoaminiwa kuchukuliwa kimakusudi ili kuonesha kuwa wanachama wote wamesimama pamoja.
Swala la Ukraine halikupigiwa upatu sana tofauti na mikutano ya kilele ya awali, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky hakushiriki katika majadiliano rasmi na viongozi wa NATO ingawa alialikwa kwenye hafla kandoni mwa mkutano huo.
Washirika wa NATO, ikiwa ni pamoja na Marekani chini ya rais wa zamani Joe Biden, walikubali mwaka jana kwamba Ukraine ilikuwa kwenye "njia isiyoweza kupingwa" kuelekea kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo ya kijeshi.
Lakini tangu Rais Trump arejee madarakani mwezi Januari, serikali yake imeweka wazi kwamba Ukraine haitajiunga na NATO katika siku za usoni na ikapunguza kwa kiasi kikubwa misaada ya kijeshi kwa nchi hiyo.
Soma pia: NATO yaahidi kuendelea kuiunga mkono Ukraine
Wakati huo huo waandamanaji na wanaharakati walionekana wakiburuzwa na kisha kukamatwa na polisi huko mjini The Hague walipokuwa wakifanya maandamano kupinga mkutano huo wa siku mbili wa viongozi wa NATO na pia shabaha yao mpya ya kuongeza matumizi ya ulinzi.
Vyanzo: DPA/AP