Namibia yarikodi kisa cha Kipindupindu baada ya muongo mmoja
14 Machi 2025Matangazo
Kisa hicho kimerikodiwa katika eneo linalopakana na Angola, ambapo mlipuko wa ugonjwa huo umewaua takriban watu 237. Haya ni kulingana na Shirika la Afya la Umoja wa Afrika.
Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika, CDC, Jean Kaseya, amesema kwa mara ya kwanza baada ya muongo mmoja, Namibia imeripoti kisa hicho cha kwanza cha ugonjwa wa kipindupindu siku mbili zilizopita.
Akiwahutubia waandishi wa habari kwa njia ya video kutoka makao makuu ya kituo cha CDC mjini Addis Ababa, Ethiopia, Kaseya amesema kuwa habari njema ni kwamba Namibia imearifu kwamba mtu huyo tayari amepona na kuondoka hospitalini.
Hata hivyo, Kaseya ameongeza kusema kuwa huo ulikuwa mwamko kwa taifa hilo kuimarisha mifumo yake katika kudhibiti ugonjwa huo.