NAIROBI : Wabunge wajichimbia bungeni kuepuka kukamatwa na polisi
30 Septemba 2005Wabunge wawili wa Kenya wamejificha bungeni hapo jana kuepuka kukamatwa na polisi ambao wanataka kuwahoji juu ya dhima yao katika kuvuruga mkutano wa mapendekezo ya katiba ambao uliishia kwa fujo.
Reuben Ndolo na David Mwenje ambao wanapinga mapendekezo hayo ya katiba na ambayo Wakenya watayapigia kura katika kura ya maoni hapo Novemba 21 wana kinga ya kutokamatwa wakati wakiwa ndani ya jengo la bunge mjini Nairobi.
Polisi inataka kuwahoji wabunge hao baada ya kuuvamia kwa ghafla mkutano ulioitishwa na wafuasi wanaounga mkono katiba hiyo hapo Jumaatano katika mkahawa ulioko kwenye jimbo la uchaguzi la Mwenje mjini Nairobi.Imeripotiwa kwamba purukushani lilizuka,viti vikarushwa na risasi zilifyatuliwa hewani.
Baadhi ya wakosoaji wanasema mapendekezo ya katiba hiyo yameshindwa kupunguza madaraka makubwa ya Rais na ni telekezo la Rais Mwai Kibaki kwa ahadi yake ya uchaguzi ya kuwashirikisha Wakenya wa fani mbali mbali na sio wanasiasa pekee katika kuandaa katiba hiyo.