NAIROBI : Uingereza yatakiwa iombe radhi kwa unyama wa ukoloni
4 Machi 2005Matangazo
Waziri wa Sheria wa Kenya Kiraitu Murungi ameitaka Uingereza kuomba radhi rasmi kwa unyama ilioutenda dhidi ya wapiganaji wa kugombania uhuru wa nchi hiyo Mau Mau wakati wa kipindi cha ukoloni.
Murungi ameitaka serikali ya Uingereza kama taifa la kistaarabu kuchukuwa uamuzi wa heshima kwa kuwaomba radhi rasmi Mau Mau,familia zao na wananchi wa Kenya kwa uhalifu wao wa kishenzi dhidi ya ubinaadamu.
Murungi alikuwa akizungumza hapo jana wakati wa uzinduzi wa kitabu juu ya kumalizika kwa utawala wa Kinyama wa Uingereza nchini Kenya kilichotungwa na Caroline Elkins wa Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani ambaye amesema kwamba mbinu zilizotumiwa na Uingereza wakati wa kuvunja uasi wa Mau Mau zilikuwa sawa na uhalifi dhidi ya ubinaadamu.