Naibu Waziri Mkuu Uingereza ajiuzulu kwa mapungufu ya kodi
5 Septemba 2025Rayner, anayefahamika kwa misimamo yake yenye muelekeo wa mrengo wa kushoto katika chama cha Labour, alikiri mapema wiki hii kwamba hakulipa kodi ya kutosha wakati aliponunua eneo la makazi kwenye jengo la ghorofa na alitoa taarifa hiyo kwa mshauri huru wa serikali anayesimamia masuala ya maadili.
Katika yake barua yake kwa Waziri Mkuu Keir Starmer mkuu wa maadili Bi Laurie Magnus alieleza kuwa Rayner alishindwa "kuzingatia tahadhari" ya ushauri wa kisheria aliyopewa na kwamba hilo linatafsirika kuwa "kanuni ya maadili imekiukwa".
Rayner mwenyewe alikubali kuwa hakutimiza viwango vya kodi vilivyohitajika alipomuandikia Starmer barua ya kujiuzulu katika nafasi za naibu waziri Mkuu, waziri wa makazi na naibu kiongozi wa Chama cha Labour
Waandamanaji wamuita Rayner "mkwepa kodi"
Kiongozi huyo alitaja kujutia mno uamuzi wake wa kutotafuta ushauri wa ziada kwa wataalam wa masuala ya ushuru huku akisisitiza kuwajibika kikamilifu kwa kosa hilo.
Hata hivyo baadhi ya waandamanaji walikusanyika nje ya nyumba ya kiongozi huyo aliyejiuzulu huku kuta za nyumba yake zikiandikwa maneno "Mkwepa kodi Rayner."
Akijibu barua hiyo ya kujiuzulu, Starmer amemueleza Rayner kuwa amehuzunishwa mno na kumpoteza mshirika huyo serikalini, lakini akaongeza kuwa atasalia kuwa muhimu katika chama cha Labour. Akizungumza bungeni, Starmer alimwagia sifa Bi Rayner huku akizomewa na wabunge wa upinzani.
"Niwe muwazi, ninajivunia mno kuona nilishirikiana na naibu waziri mkuu ambaye alijenga nyumba milioni 1.5 ambaye ameboresha kwa kiasi kikubwa haki za wafanyakazi kwa miaka mingi na ambaye anatokea kwenye tabaka la wafanyakazi na baadae akaja kuwa naibu waziri mkuu wa nchi hii."
Kujiuzulu kwa Rayner kunazidisha masaibu serikalini
Kujiuzulu Kwa Rayner kunazidisha masaibu kwenye serikali ya Starmer, ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi tangu iingie madarakani mnamo Julai mwaka 2024, baada ya miaka 14 katika upinzani.
Uingereza imelazimika kubadili msimamo wake kwenye masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na mageuzi ya mfumo wa ustawi na mafao ya wazee huku kitendo cha serikali ya Starmer kushindwa kukabiliana ipasavyo na ujio mkubwa wa wahamiaji wasio na vibali wanaowasili kwa mashua, hatua inayochochea uungwaji mkono wa umma kwa chama cha mageuzi cha Nigel Farage kinachofahamika zaidi kama Reform UK.
Kulingana na kura za maoni nchini Uingereza, chama cha Labour cha Waziri Mkuu Keir Starmer kipo nyuma ya kile cha Reform UK chake Nigel Farage ingawa uchaguzi mkuu ujao huenda hautofanyika kabla ya mwaka 2029.