Mzozo wa Sudan unasambaa hadi Jamhuri ya Afrika ya Kati
27 Juni 2025Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Operesheni za Amani Jean-Pierre Lacroix ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa shambulizi lililomuuwa mlinda amani wa Umoja wa Mataifa karibu na mpaka wa nchi hiyo na Sudan Ijumaa iliyopita lilifanywa na "washambuliaji kutoka Sudan".
Matamshi yake ndio ya kwanza yanayowataja wapiganaji wenye silaha kutoka Sudan kuwa ndio waliohusika na shambulizili hilo dhidi ya walinda amani. "Ninalaani vikali shambulio hili na natoa rambirambi zangu za dhati kwa familia ya mwathiriwa, pamoja na serikali ya Zambia. Narudia wito wangu kwa mamlaka za Afrika ya Kati kufanya kila liwezekanalo kuchunguza kilichotokea na kuwawajibisha wahusika wa shambulio hili baya."
Sudan ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe wakati majenerali wanaopingana, wanaoongoza vikosi vya jeshi la taifa na wanamgambo wa RSF walianza kupigana katikati ya mwezi Aprili 2023. Tangu wakati huo, watu 24,000 wameuawa, karibu Wasudan milioni 13 wamekimbia makaazi yao, baa la njaa linakaribia na kipindupindu kimeshuhudiwa nchi nzima. Pande zote zinatuhumiwa kwa uhalifu wa kivita.
Wakati huo huo, Jamhuri ya Afrika ya Kati imekuwa ikikabiliwa na mzozo tangu mwaka wa 2013, wakati waasi wengi wao kutoka jamii ya Waislamu walikamata Madaraka na kumuondoa aliyekuwa rais wakati huo Francois Bozize.
Lacorix, amesema kuwa wakati hatua zinapigwa na baadhi ya makundi katika kuutekeleza mpango wa amani nchini humo, machafuko kati ya makundi yenye silaha na wapiganaji yanaendelea. Hiyo amesema inahujumu utulivu na kuwa kitisho kwa raia.
Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kwenye Umoja wa Mataifa Marius Aristide Hoja Nzessioué, alisisitiza ujumbe huo akielezea dhamira ya serikali kwenye mazungumzo. "Mazungumzo ya kisiasa ambayo yanapangwa na mamlaka za Afrika ya Kati hayaanzishwi kwa amri ya nje. Hili ni jibu la ombi rasmi lililotolewa na upande wa upinzani wa Republican, haswa wanachama wa BRDC. Katika kujibu ombi hili, Rais wa Jamhuri kimsingi alitoa idhini yake, na hivyo kuonyesha nia yake ya kushiriki katika mazungumzo ya kisiasa."
Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati inaendelea kushirikiana na Jeshi la Kulinda Amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati – MINUSCA kuhusu kurefushwa na kuimarisha uwepo wake kote nchini humo na kuboresha usalama kwenye maeneo ya mipaka.
Lacroix amesema huku uchaguzi mkuu ukitarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu, hali ya kisiasa inaendelea kufunikwa na kiwingu cha kutoaminiana na hofu kati ya wengi walioko madarakani na upinzani. Ameongeza kuwa uchaguzi huo unatoa fursa ya muhimu ya kuimarisha uongozi wa kidemokrasia, kukuza maridhiano na kuweka mazingira bora ya utulivu.
AFP