Mzozo wa mpakani Thailand na Cambodia wazidi makali
26 Julai 2025Watu wasiopungua 33 wameuawa na zaidi ya 168,000 wamelazimika kuyakimbia makaazi yao. Shinikizo la kimataifa linaongezeka kwa pande zote mbili kufikia makubaliano ya kusitisha uhasama.
Mashambulizi ya makombora na risasi yameripotiwa karibu na vijiji kadhaa vilivyopo eneo la mpaka wa baina ya nchi hizo mbili, hali inayotanua eneo la mapigano tangu uhasama ulipozuka Alhamisi iliyopita.
Siku hiyo bomu la kutegwa ardhini lililipuka na kuwajeruhi wanajeshi watano wa Thailand. Kila upande umedai umechukua hatua ya kulipa kisasi kwa matendo yaliyofanywa na mwingine.
Nchi zote mbili zimewaondoa mabalozi wake na Thailand imevifunga vituo vyote vya mpaka wake wa kaskazini mashariki na Cambodia.
Mamlaka nchini Cambodia zimetangaza vifo vingine vya watu 12, na kufikisha idadi jumla ya vifo 14 wakati maafisa wa Thailand wamesema mwanajeshi wake mmoja ameuawa siku ya Jumamosi na kufanya idadi jumla upande huo kufikia vifo 20.
Jumuiya ya ASEAN yashinikizwa kutafuta suluhu
Jumuiya ya kikanda ya mataifa ya kusini mashariki mwa bara la Asia, ASEAN, inakabiliwa na shinikizo la kutafuta sukuhu kati ya nchi hizo mbili wanachama.
Kwenye mkutano wa dharura ulioitishwa siku ya Ijumaa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limeitolea mwito jumuiya ya ASEAN kusuluhisha mgogoro kati ya Thailand na Cambodia.
Eneo la mpaka kati ya nchi hizo mbili lenye ukubwa wa kilometa 800 limekuwa linagombaniwa kwa miongo mingi.
Makabiliano ya siku zilizopita yalikuwa madogo na ya muda mfupi. Msuguano uliopo sasa ulizuka mwezi Mei pale mwanajeshi wa Cambodia alipouawa kwenye makabiliano na kuchochea mvutano wa kidiplomasia.
Wizara ya Ulinzi ya Cambodia imekosoa kile imekitaja kuwa kutanuka kwa mashambulizi ya Thailand mapema siku ya Jumamosi.
Imesema makombora makubwa matano yalivurumishwa na Thailand kuyalenga maeneo tofauti ya jimbo la Pursat, na kulitaja shambulizi hilo kuwa "kitendo kisichotokana na uchokozi na kilichopangwa makusudi."
Kila upande waulaumu mwingine kuwa chanzo cha mgogoro
Msemaji wa wizara hiyo ya Cambodia Luteni Jenerali Maly Socheata amesema makabiliano yamezuka kwenye jimbo la Koh Kong, eneo ambako boti nne za kijeshi za Thailand zimeonekana zimetia nanga na nyingine 4 zikiwa safarini. Amesema kupelekwa kwa zana za kijeshi ni "kitendo cha uchokozi" na kunatishia kuongeza msuguano.
Maly Socheata amesema raia 7 na wanajeshi watano wameuawa ndani ya siku mbili za mapigano. Mapema siku ya Jumamosi, mwanaume mmoja aliripotiwa kuuawa baada ya jengo alimokuwa amejificha kushambuliwa na makombora ya Thailand.
Jeshi la Thailand limekanusha madai ya kuyalenga maeneo ya kiraia ndani ya Cambodia na badala yake limeituhumu serikali mjini Phnom Penh kuwatumia raia "kama kinga" kwa kuweka silaha zake kwenye maeneo yaliyo jirani na maakazi ya watu.
Wakati huo huo, jeshi la wanamaji la Thailand, kwenye taarifa yake iliyotolewa siku ya Jumamosi, limevituhumu vikosi vya Cambodia kwa kuanzisha mashambuli mapya kwenye mkoa wa Trat, lakini limejinasibu kuwa limefanikiwa kujibu hujuma hizo na kuzima uvamizi wa vikosi vya Cambodia kwenye maeneo matatu ya kimkakati.
Jeshi hilo limeapa kuwa "uchokozi hautafumbiwa macho."