Mzozo wa Kongo wasababisha janga la njaa kwa watoto
7 Aprili 2025Kulingana na tathmini ya takwimu mpya za vipimo na viashiria vya kimataifa vya uhaba wa chakula-Integrated Food Security Phase Classification,IPC- idadi ya watoto wanaokabiliana na uhaba mkubwa wa chakula katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, imeongezeka kutokea milioni 12.3 hadi 14.6 hadi kufikia Januari ikilinganishwa na kipindi hichohicho mwaka uliopita.
Takwimu zinaashiria kuwa mtoto mmoja kati ya wanne anahangaika kupata chakula kote nchini humo.
Baa hilo ni baya zaidi katika maeneo yaliyozongwa na vita ya mashariki ya Ituri, Kivu ya Kaskazini na Kusini na Tanganyika.
Utafiti wa shirika la kuwahudumia watoto la Save The Children umebaini kuwa idadi ya watoto walioathirika imeongezeka kwa asilimia 47 ikilinganishwa na kipindi hicho cha Januari hadi Juni mwaka uliopita wa 2024.
Chanzo cha kusababisha hali hiyo ni vita vinavyoendelea kadhalika mapambano ya moja kwa moja tangu mwanzoni mwa mwaka.
Soma pia:Baraza la Usalama la UN kuchukuwa hatua kali dhidi ya Kongo
Shelley Thakral ni msemaji wa Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa,WFP katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na anasisitiza kuwa hali inatisha.
"Tulichokiona katika muda wa miezi sita iliyopita ni kuwa watu milioni 2.5 wa ziada wamesukumwa na kuwa kwenye kundi la wanaokabiliana na uhaba mkubwa wa chakula."
Aliongeza kwamba wakaazi wa eneo la mashariki tayari wanatatizwa na changamoto kadhaa na miezi sita iliyopita imekuwa ya mazingira magumu na kupoteza hata tumaini.
"Ongezeko la bei za vyakula linawahatarisha zaidi wanawake na watoto….aghalabu wanyonge ndio wanaoumia zaidi.Familia ambazo zimekuwa zikihangaika kupata chakula,sasa zinakabiliana na ugumu na uhalisia mpya.”
Zaidi ya watu milioni tatu wanatafuta hifadhi
Katika miezi michache iliyopita, kiasi ya watu milioni 3 wamekuwa njiani wakisaka sehemu salama kwasababu ya mapigano au kujaribu kurejea makwao, hali inayotatiza juhudi za kupata rizki ya kila siku.
Kwa mujibu wa takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, kwa sasa watu milioni 6.4 wameachwa bila makaazi kutokana na vita huko Kongo na zaidi ya nusu ya idadi hiyo wako kwenye majimbo ya Kivu ya Kusini na Kaskazini pekee.
Soma pia:Watu milioni 282 duniani walikumbwa na njaa kali mwaka 2023
Uhaba au ukosefu wa chakula una madhara makubwa kwa afya ya watoto hali inayoleta utapia mlo, mwili kudumaa, mifumo ya kinga hafifu na kuongeza uwezekano wa kupata magonjwa.
Kadhalika, watoto wasiopata chakula cha kutosha na lishe, hupitia kipindi kigumu kwenye masomo hata ikiwa wanayo nafasi ya kwenda shule.