Mzozo wa Israel na Iran waingia wiki ya pili
20 Juni 2025Israel na Iran ziliendelea kushambuliana hapo jana Alhamisi na usiku wa kuamkia leo katika wakati ishara za kutumika diplomasia zinachomoza ili kumaliza makabiliano hayo ya nchi hizo mbili hasimu yaliyotimiza wiki nzima.
Hapo jana ndege za kivita za Israel ziliyashambulia maeneo kadhaa ndani ya Iran ikiwemo kituo cha kutengeneza kiminikika maalamu cha kupooza vinu vya nyuklia.
Iran ilijibu mapigo kwa kuushambulia kwa makombora ya masafa mji wa Tel Aviv na mji wa kusini mwa Israel wa Beer Sheva. Kwenye shambulizi la Beer Sheva hospitali katikati mwa mji huo ililengwa hayo ikiwa ni kulingana na taarifa kutoka ndani ya Israel.
Viongozi wa Israel wameghadhibishwa na shambulizi hilo wakiituhumu Iran kuyalenga maeneo ya kiraia lakini Tehran imejibu ikisema shambulizi lake halikuilenga "hospitali bali kamandi ya kijeshi iliyokuwa karibu na jengo hilo."
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliapa kuwa "watawala mjini Tehran watalipa kwa shambulizi hilo lililoharibu hospitali ya Soroka" na kujeruhi watu wapatao 240.
Usiku wa kuamkia leo Israel ilitoa indhari kwa watu wa kijiji kimoja cha kaskazini mwa Iran kuondoka eneo hilo huku ripoti zikisema pia ilifanya mashambulizi ndani ya mji mkuu wa Iran, Tehran.
Trump ajipa wiki mbili za kuamua kuhusu kuingia kijeshi Iran
Hayo yakijiri, Rais Donald Trump ambaye anaandamwa na miito kutoka kwa Israel ya kumtaka asaidie kuishambulia miundombinu ya nyuklia ya Iran, amesema anajipa muda wa wiki mbili kuamua iwapo Washington itachukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran ama la.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani ndiye ametoa taarifa hizo usiku wa kuamkia leo akinukuu ujumbe alotumiwa moja kwa moja na Rais Trump.
Kulingana na msemaji huyo Karoline Leavitt, Trump amechukua uamuzi huo kupisha nafasi ya mazungumzo ya kidiplomasia yanayoweza kufanyika kati ya Iran na Marekani.
Inaaminika Israel inataka Marekani isaidie kukishambulia kinu cha nyuklia cha Iran cha Fordo kilichojengwa umbali mrefu chini ya ardhi.
Ni Marekani pekee inatajwa kuwa na uwezo wa kijeshi wa kukisambaratisha kituo hicho cha nyuklia kwa kutumia bomu maalumu la kutifua ardhi hadi umbali wa futi 60.
Vyanzo kadhaa vimearifu kuwa Iran na Marekani wameendelea kuwa na mawasiliano hata baada ya Israel kuishambulia nchi hiyo ya kiislamu wiki iliyopita.
Taarifa zinasema Mjumbe Maalumu wa Marekani kwenye kanda ya Mashariki ya Kati amefanya mazungumzo mara kadhaa na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araghchi.
Diplomasia inaweza kunusuru maafa zaidi mzozo wa Israel na Iran?
Waziri Abbas Araghchi wa Irana hivi leo anaelekea mjini Geneva kwa mkutano na wenzake wa Ujerumani, Uingereza na Ufaransa ikiwa ni mara ya kwanza kwa mkutano wa ngazi ya juu kufanyika kati ya maafisa wa Iran na nchi za magharibi tangu Iran iliposhambuliwa na Israel wiki iliyopita.
Inatazamiwa wazungumzo ya wanadiplomasia hayo yatatuama juu ya kutuliza mivutano na kuishinikiza Iran kuachana na mradi wake wa nyuklia unaoelezwa kuwa sababu ya Israel kuilenga nchi hiyo.
Iran imesisitiza mara kadhaa kuwa mradi wake huo ni matumizi ya kiraia lakini Israel na Marekani zinaamini watawala mjini Tehran wanalenga kuutumia kuunda bomu la nyuklia.
Maafisa kadhaa wa Iran wamejitokeza kumshambulia Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Silaha za Nyuklia IAEA, Rafael Grossi wakimtuhumu kuwa chanzo cha mzozo wa sasa kwa kushindwa kusema kinagaubaga kuwa Iran haina mpango wa kuunda silaha za nyuklia.