Mzozo juu ya mpango wa Nuklia wa Iran waendelea
6 Septemba 2005Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Javier Solana amezitaka Iran pamoja na Korea Kaskazini kurejea katika meza ya mazungumzo juu ya mipango yao ya Kinulia.
Solana akiwa Beijing amesema Umoja wa Ulaya uko tayari kurejelea tena mazungumzo na Iran kwa ajili ya kuleta uhusiano mpya wa kisiasa na kiuchumi na taifa hilo.
Javier Solana aliyasema hayo baada ya kumalizika kwa mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na China mjini Beijing.
Lakini hata hivyo Solana ameongeza kusema kuwa ni hiyari ya Iran kukubaliana na wazo hilo.
Iran imo katika hali ya mgongano na jumuiya ya Ulaya baada ya kurejelea mpango wake wa kurutubisha madini ya Uranium ambapo inahofiwa huenda ikaanza kutengeneza mabomu ya Atomiki.
Hata hivyo licha ya serikali ya Iran kudai kwamba mpango wake wa kinuklia ni kwa ajili ya matumizi yake ya amani,Uingereza ,Ufaransa na Ujerumani zimekuwa zikijaribu kuishawishi Iran iachane kabisa na mpango wa kutengeneza mafuta ya Nuklia.
Upande wake Solana amesema kwa Umoja wa Ulaya suala muhimu ni kuhakikisha Iran haitumii mpango wake wa kinuklia kutengeneza silaha hatari za Nuklia.
Nchi tatu za Umoja wa Ulaya ikiwa ni Ujerumani,Uingreza na Ufaransa mwishoni mwa mwezi July ziliitaka rasmi Iran kuachana na mpango unaohusiana na urutubishaji madini ya Uranium na badala yake ikubali usaidizi wa kibiashara,na kupata mafuta ya nuklia kutoka mataifa ya nje na vile vile kusaidiwa katika hali ya kiusalama na mataifa hayo.
Lakini mataifa hayo yalishindwa kuishwishi Iran barabara kwani nchi hiyo ilirejelea mpango wake wa Nuklia katika mtambo wake wa Isfahan mnamo Agosti 8.
Hadi kufikia sasa Iran imekataa katakata kubadili msimamo wake na wala haijatoa hakikisho lolote juu ya kuachana na mpango wake na pamoja na hayo Iran haijazingatia kikamilifu maagizo ya bodi ya magavana wa shirika la Kimataifa la Umoja wa Mataifa linalodhibiti matumizi ya nishati ya Atomiki IAEA.
Awali Solana alisema Umoja huo wa Ulaya hauna njia nyingine ya kuchukua isipokuwa tu ,kulipeleka suala hilo mbele ya baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Sasa Solana anasema amelijadili suala la Iran pamoja na Korea Kaskazini katika mkutano wake na viongozi wa China.
Amesema hii ni kutokana na kuwa China inakabiliwa na tatizo hilo hilo kutoka upande wa Korea kaskazini kukataa kufika kwenye kikao cha mataifa sita juu ya mpango wake wa Nuklia.
Wakati huo huo Russia nayo imepinga pendekezo la kuipeleka Iran mbele ya baraza la usalama la umoja wa mataifa ili kuwekewa vikwazo juu ya mpango wake wa Nuklia.
Hatua hiyo ya Russia inaonekana kana kwamba ni ya kujitumbukiza katika mgongano na Marekani katika chombo hicho muhimu duniani ambapo Russia pia inashikilia kura ya turufu katika chombo hicho.
Russia ambayo imekuwa ikikosolewa kwa muda mrefu na Marekani kwa kuitengenezea Iran mtambo wa Nuklia ni mwanachama wa kudumu katika baraza hilo na ina uwezo wa kura ya turufu wa kuzuia suala la Iran lisifikishwe mbele ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa.
Ujerumani ambayo ni mshirika wa karibu wa Russia inaonekana kulemea zaidi upande wa Russia ikisema jambo muhimu litakaloweza kuumaliza mzozo juu ya Iran ni kufanyika tena mazungumzo hayo kati ya Iran ,Shirika la kimataifa la umoja wa mataiafa la kudhibiti nguvu za Atomiki na Umoja wa Ulaya.
Wolfgang Gerhaedt ambaye huenda akawa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani baada ya uchaguzi wa septemba 18 amesema mazungumzo juu ya suala la Iran hivi sasa sio mada katika baraza la usalama la umoja wa mataifa isipokuwa mazungumzo yanafaa kufufuliwa tena ili kuishawishi nchi hiyo isiendelee na mpango wake wa Nuklia.
Iran imekanusha dhamira mbaya juu ya mpango wake wa Nuklia kama inavyodai Marekani na Umoja wa Ulaya inasema imeyajibu maswali yote iliyoulizwa na shirika hilo la kudhibiti matumizi ya Atomiki duniani IAEA na kuwa imeonyesha wazi kwamba nia yake ni tu ya kutengeza Nuklia kwa ajili ya kuzalisha nguvu za umeme.
Wanadiplomasia nchini Russia wamearifu kwamba msimamo wa Russia juu ya Iran unatokana na hofu ya kupoteza mshirika wa karibu katika mashariki ya kati na soko muhimu la technologia yake ya kinuklia.
Russia imeijengea Iran mtambo wa nuklia wa gharama ya dolla bilioni moja katika eneo la Bushehr ambao unatarajiwa kufunguliwa rasmi mwakani na hivyo basi Russia inataka ushirikiano zaidi wa kibishara na Iran.