Myanmar yaomboleza baada ya tetemeko la ardhi
31 Machi 2025Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya uongozi wa Myanmar, kipindi hicho rasmi cha maombolezo ya taifa kitaendelea hadi tarehe 6 mwezi wa Aprili. Bendera zinapepea nusu mlingoti ili kuwakumbuka waliopoteza maisha yao kwenye tetemeko hilo la mwishoni mwa wiki iliyopita. Wakaazi wanaripotiwa kupoteza tumaini wakati juhudi za uokoaji zikiendelea.
Baadhi wamelazimika kulala nje kwa siku ya tatu mfululizo tangu mkasa huo kutokea na kuitikisa nchi jirani ya Thailand. Kwa siku ya Jumatatu, juhudi za uokoaji zilipungua kasi katikati ya mji wa Myanmar kwani hali ni ngumu ukizingatia kuwa viwango vya joto vinaongezeka na kukadiriwa kufikia 40 katika viwango vya celsius.
Idadi ya walioangamia kufuatia tetemeko la ardhi Myanmar inazidi kupanda
Joto hilo linawatatiza waokoaji kadhalika maiti kuoza jambo litakaloifanya shughuli ya kuzitambua kuwa ngumu zaidi. Afisa wa Idara ya zimamoto wa Myanmar ambaye hakutaka kutajwa jina amesema ikiwa mwathirika atapatikana baada ya saa 72 kwenye eneo dogo chini ya vifusi - kuna uwezekano mdogo wa kukutwa akiwa hai, lakini kwa bahati nzuri akikutwa hai, bila bila shaka, taifa litatumia uwezo wote ulio nao ili kujaribu kuwaokoa.
Tetemeko la ardhi laharibu majengo na miundombinu
Wakati huohuo, waislamu walioko eneo hilo walikusanyika karibu na msikiti mmoja uliobomolewa ili kuswali kwa sikukuu ya Eid Ul Fitr baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhan kukamilika. Kadhalika, mamia wanatarajiwa kuzikwa siku ya Jumatatu.Tetemeko la ardhi la kwanza lililiponda eneo la Mandalay Ijumaa mchana likiwa na vipimo vya 7.7 vya Richter kisha baadae mtikisiko ukalikumba eneo hilo.
Hali hiyo iliporomosha majengo, kuvunja madaraja na barabara kubomoka ikiwa ni uharibifu ambao haujawahi kushuhudiwa. Mitikisiko ya mwishoni mwa wiki iliwasukuma wakaazi kulikimbia eneo la Mandalay kwa hofu. Kwa upande wake, shirika la misaada la msalaba na hilal nyekundu limewasilisha ombi jipya la kuchangisha zaidi ya dola milioni 100 za Marekani kuwaokoa wahanga wa tetemeko hilo la ardhi.
Tetemeko: Juhudi za uokoaji zaendelea Myanmar na Thailand
Kulingana na shirika hilo lililo na mtandao mkubwa zaidi wa kusambaza misaada ya kibinadamu kote duniani, mahitaji ni makubwa kwani joto linaongezeka na msimu wa mvua unawadia kwa hiyo uwezekano wa majanga mengine kutokea unaongezeka.
afp/ap/reuters