Guterres atoa wito wa kukabiliana na ukosefu wa makaazi
30 Mei 2025Guterres amesema jamii ya kimataifa imo kwenye njia panda katika harakati za kudhibiti ongezeko kubwa la idadi ya watu wasio na makazi duniani.
"Hatuwezi kuwa na dunia yenye maisha bora endapo watu hawatokuwa na makao bora, huku wengine wakiwa wamekwama kwenye maisha ya ufukara wakiishi katika vitongoji duni", amesema Guterres.
Ni kutokana na hilo, ambapo zaidi ya wajumbe 1,200 kutoka nchi-193 wanachama wa Umoja huo wanashiriki katika kikao hicho cha siku mbili cha baraza la shirika la makazi ili kutafuta ufumbuzi mwafaka wa tatizo hilo.
Akihutubia kikao hicho cha ngazi ya juu cha baraza hilo, mkurugenzi mtendaji wa shirika la makazi duniani, UN Habitat, Anacláudia Rossbach, amesema ajenda mpya ya mwaka 2026-2029 inajikita katika kutatua tatizo la ukosefu wa makazi ulimwenguni.
"Kwa sasa, zaidi ya watu bilioni 2.8 wangali wanaishi katika makazi duni, huku wengine zaidi bilioni 1 wakiishi katika mitaa ya mabanda, ilhali zaidi ya watu milioni 300 hawana makao."
"Tumepea kipaumbele ujenzi wa nyumba za bei nafuu"
Miongoni mwa wanaohudhuria kongamano hilo ni mawaziri wa serikali za nchi mbalimbali, na wajumbe kutoka mashirika ya umma na sekta ya kibinafsi. Alice Wahome ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Miji kutoka Kenya amesema kipaumbele ni makaazi ya bei nafuu.
"Tumepea kipaumbele ujenzi wa nyumba za bei nafuu, kuboresha miundombinu ya miji yetu, na kuwezesha jamii kama nguzo muhimu ya kuimarisha ajenda ya maendeleo ya taifa."
Mkutano huo umewadia wakati ambapo bara la Afrika linashuhudia ongezeko kubwa tena la haraka mno la idadi ya wakazi wa mijini.
Miongoni mwa ajenda kuu za mkutano huo ni uwepo wa makazi bora ya gharama nafuu, uzuiaji uchafuzi wa hewa mijini, na utekelezaji wa sera na malengo ya maendeleo endelevu miongoni mwa nchi wanachama.
Kikao cha baraza hilo kitafikia kilele chake kesho Ijumaa huku wajumbe na washiriki wakitazamia kupitisha maazamio mbalimbali kwa lengo la kuboresha hali ya makaazi mijini, hasa katika mataifa yanayoendelea.