Mwili wa Papa Francis wawasili Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro
23 Aprili 2025Ni kwa nyimbo za ibada huku Kengele za Kanisa la Mtakatifu Petro zikilia, ndivyo jeneza la mbao na la wazi la Papa Francis lilibebwa katikati ya umati wa watu waliojaa katika uwanja wa kanisa hilo wakisindikizwa na makadinali waliovalia mavazi mekundu na kusindikizwa na Walinzi wa Vatican wanaofahamika zaidi kama "Vikosi vya Uswisi".
Waumini, mahujaji na watalii walipiga picha za ukumbusho, huku wengine wakipiga makofi kama ishara ya heshima kwa Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki wakati msafara huo ukipita kutoka kwenye makazi ya Mtakatifu Marta, ambapo papa huyo raia wa Argentina mwenye umri wa miaka 88 alifariki Jumatatu baada ya maradhi ya muda mrefu na ambako aliishi kwa miaka 12 ya uongozi wake.
Soma pia: Watu wamiminika Vatican kumuaga Papa Francis
Mauro raia wa Italia na Jose Rojo kutoka Mexico ni miongoni mwa walioshuhudia jeneza hilo la Papa Francis likiwasili katika kanisa la Mtakatifu Petro siku ya Jumatano na walikuwa na haya ya kusema:
" Binafsi nilimchukulia kama mtu ambaye aliwakilisha enzi za mabadiliko kwa imani ya Kikristo ambayo tunapaswa kudumisha, na ndiyo sababu sikuweza kuikosa fursa hii."
" Nimejawa na hisia ya huzuni kuona kwamba papa hayuko nasi tena. Papa alikuwa karibu sana na vijana pamoja na watu wa Amerika ya Kusini."
Papa Francis kuzikwa mjini Roma Jumamosi
Mazishi ya Papa Francis siku ya Jumamosi yanatarajiwa kuhudhuriwa na mamia kwa maelfu ya mahujaji pamoja na viongozi wa dunia akiwemo Rais wa Marekani Donald Trump, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na hata Mwanamfalme William wa Uingereza. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Italia Matteo Piantedosi amesema wanatarajia wajumbe kutoka nchi za nje wapatao 150 hadi 170 pamoja na maelfu ya watu.
Soma pia: Viongozi wa dunia wajiandaa kushiriki mazishi ya Papa Francis
Baadaye, jeneza la Papa Francis litapelekwa katika Kanisa alilolipenda zaidi la Mtakatifu Maria Maggiore mjini Roma, ambako atazikwa na kaburi lake kuandikwa Franciscus. Mamlaka za Italia zinajiandaa na operesheni kabambe ya usalama kwa ajili ya mazishi ya Papa Francis huku siku ya Ijumaa ikitangazwa kuwa likizo ya kitaifa.
Tayari vizuizi kadhaa vimewekwa ndani na nje ya Kanisa la Mtakatifu Peter ili kudhibiti umati wa watu ambao tayari umewasili eneo hilo, huku ukaguzi na usalama vikiimarishwa na wafanyakazi wakiwapatia watu chupa za maji kutokana na jua linaloshuhudiwa huko Vatican.
(Vyanzo: DPA, AFP, Reuters, AP)