Mhafidhina ashinda duru ya kwanza uchaguzi wa rais Romania
5 Mei 2025Kwenye uchaguzi huo, Simion wa chama cha Alliance for the Unity of Romanians (AUR), amejikingia asilimia 40.5 ya kura akiwazidi kwa umbali mkubwa wapinzani wake, ikiwemo Meya wa mji mkuu Bucharest Nicusor Dan aliyeshika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 20.89 ya kura.
Kulikuwa na wagombea 11 kwenye uchaguzi huo na duru ya pili kutafuta mshindi atakayepata zaidi ya asilimia 50 itafanyika Mei 18.
Uchaguzi huo ulikuwa ni wa marudio baada ya ule uliofanyika Disemba mwaka uliopita kubatilishwa na Mahakama ya Juu ya nchi hiyo kufuatia madai ya kuingiliwa na ushawishi wa Urusi, suala ambalo Moscow ilikanusha.
Kufutwa kwa uchaguzi huo kuliitumbukiza Romania, taifa mwanachama wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami ya NATO kwenye mzozo mkubwa wa kisiasa kuwahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa.