Mwanaharakati wa Kenya anashikiliwa Tanzania
20 Mei 2025Mwangi, alikuwa miongoni mwa wanaharakati wengine wa Afrika Mashariki waliosafiri kwenda Tanzania siku ya Jumatatu kwa ajili ya kuhudhuria kesi ya uhaini ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu, katika kuonyesha mshikamano kwa kiongozi huyo.
Mke wa Mwangi, Njeri ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa, AFP kuwa hajafanikiwa kuwasiliana na mumewe tangu alipokamatwa.
Njeri amesema amearifiwa kuwa wanasubiri serikali ya Tanzania kushauriana na kuamua kama imfungulie mashtaka au kumfukuza nchini humo.
Mwangi alikamatwa katika Hoteli ya Serena pamoja na mwanaharakati wa Uganda, Agather Atuhaire.
Wanaharakati kadhaa, akiwemo mgombea wa urais wa Kenya, Martha Karua, walikataliwa kuingia nchini humo mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege na walirudishwa.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alisema Jumatatu kuwa wanaharakati wa kigeni hawatoruhusiwa kuingilia masuala ya nchi hiyo, na kuvitaka vyombo vya usalama kutoruhusu wale aliowaita "watovu wa nidhamu" kutoka mataifa mengine kulichafua taifa hilo.