Alon Pinkas: Hali ndani ya Israel haiakisi demokrasia
28 Machi 2025Pinkas amesema uamuzi wa hivi karibuni wa serikali ya Netanyahu wa kumfuta kazi Mkuu wa Shirika la Ujasusi la ndani la Shin Bet, Ronen Bar na nia ya kumfukuza Mwanasheria Mkuu wa Serikali hauendani na demokrasia kwa namna yoyote.
Aliyewahi kuwa balozi wa Israel nchini Marekani Alon Pinkas amemkosoa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akisema kuwa kiongozi huyo anataka jukumu lake katika shambulio la Oktoba 7 mwaka 2023 lililofanywa na wanamgambo wa Hamas lisahaulike katika historia ya Israel.
Pinkas ambaye pia alikuwa mshauri wa kisiasa wa mawaziri wakuu wawili wa zamani Shimon Peres na Ehud Barak ameyasema hayo katika mahojiano maalumu na shirika la habari la DW. Ameeleza kuwa kadri Netanyahu anavyozidi kusalia madarakani ndivyo anavyojitenga na tukio hilo.
Zaidi Pinkas amemfananisha Netanyahu na baadhi ya viongozi aliowataja kuwa ni madikteta akisema kuwa, "Kiongozi yeyote wa kiimla; Viktor Orban wa Hungary, Erdogan wa Uturuki, Trump wa Marekani, Duterte aliyekuwa Rais wa Ufilipino au Bolsonaro huko Brazil- wanajiita wananamageuzi wanaofuata demokrasia, suala linalomaanisha ni watawala wa kiimla na ni kama alivyo Bwana Netanyahu."
Soma zaidi: Maandamano dhidi ya Netanyahu yafanyika Israel
Siku kadhaa zilizopita Netanyahu alianzisha mchakato wa kumfukuza Mkuu wa shirika la ujasusi la ndani la Shin Bet Ronen Bar ambaye amedai kuwa hana imani naye lakini hatua hiyo ilizuiwa na mahakama kuu Ijumaa iliyopita. Ameonesha pia nia ya kutaka kumfuta kazi mwanasheria mkuu wa serikali.
Pinkas Alipoulizwa na mwandishi wa DW Brent Goff kuhusu hali ya uwajibikaji inavyoweza kuwa kama maafisa hao watafutwa kazi amejibu kuwa hilo ni tatizo kwa kuwa vyombo vya kuhakikisha uwajibikaji vinaelekea kuanguka na kuwa mfumo wa kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi unasambaratishwa na Netanyahu.
Amezitaja nguzo za uwajibikaji nchini humo kuwa moja wapo ni mahakama kuu ambayo amesema haiwezi kukurupuka siku moja na kufanya maamuzi ya ghafla. Ameielezea nguzo ya pili kuwa ni umma wa Israel ambao umekuwa ukifanya maandamano kwa muda mrefu lakini umeonekana zaidi mwaka mmoja baada ya Oktoba 7, 2023.
Pinkas amshutumu Netanyahu kwa kuvunja sheria
Zaidi amemkosoa Netanyahu, na kusema kuwa Netanyahu anajiona kama aina fulani ya mlinzi na mkombozi ya Israel na anafikiri kuwa Israel inapaswa kumshukuru kwa uongozi wake uliotukuka na pale Israel anapoonekana kutokufurahishwa au kutokuridhishwa basi kiongozi huyo huvunja kanuni."
Raia nchini Israel wamekuwa wakifanya maaandamano ya kuikataa serikali ya Netanyahu kutokana na namna anavyoushughulikia mzozo kati ya nchi hiyo na kundi la Hamas ambalo bado linawashikilia mateka kadhaa wa Israel. Jumatano wiki hii, waandamanaji wanaoipinga serikali yake walijikusanya karibu na bunge la Israel kupinga muswada utakaoongeza ushawishi wa kisiasa kuhusu uteuzi wa mahakimu. Miongoni mwa waliozungumza kwenye maandamano hayo walitoa wito wa kuachiliwa kwa mateka na kwa Israel kuanza mazungumzo ya usuluhishi ili kusitisha vita Gaza.
Alon Pinkas amesema kura ya maoni ya hivi karibuni nchini Israel inaonesha kuwa kama uchaguzi ungefanyika sasa Netanyahu angeshindwa kutetea kiti chake bila kujali ni nani anayegombea dhidi yake.
Ameeleza kuwa Waziri Mkuu huyo anaendezela vita na kukiuka katiba ili aendelee kusalia madarakani. Amesisitiza kuwa licha ya Netanyahu kujitenga na jukumu lake katika shambulio la Oktoba 7, 2023 anajua kuwa historia itamhukumu.