Mwaka mmoja tangu kutoweka wanaharakati wa CHADEMA
20 Agosti 2025Deusdedith Soka, kama walivyo vijana wengi Tanzania yumkini alikuwa na ndoto lukuki za kuyapatia maisha kiuchumi, kisiasa na katika jamii yake, lakini tangu kutoweka kwake Agosti mwaka jana, ndoto hizo ni kama zimeyeyuka mithili ya barafu kwenye moto.
Soka, akiwa na umri wa miaka 29 tu. Alikuwa kiongozi wa kambi ya vijana wa Chadema(BAVICHA) nafasi aliyoisimamia vyema na kuonyesha safari yenye kutia hamasa ya mwanasiasa kijana. Kabla ya kutoweka kwake, alisema haya:
Lissu akutwa na kesi ya kujibu kuhusu uhaini
"Nataka niwaaambie siku mkisikia nimepotea mjue ni polisi, nafanya kazi zangu za harakati kuhakikisha nchi yangu inakuwa huru na haki."
Hata hivyo kutoweka kwake kumeacha fumbo kwa wanafamilia ambao wanajiuliza, wakisema, hawana nguvu tena ya kumpata Deus, kama wanavyomwita. DW imezungumza na baba mdogo wa Deusdedith, Didas Soka.
"Sisi kama familia tuliwahi kuitwa Chadema ili wanaharakati wa haki za binadamu watuhoji, lakini mpaka sasa haki za binadamu hawajawahi kurudi kwetu kutusaidia, sisi kama familia tunasikitika sana, tunasikitiika mnoo, nitoe wito kwa serikali, kama huyu kijana yupo tunamuomba, kama hayupo basi watuletee mwili wake kwa sababu kila kabila zina taratibu za kuzika”
Sambamba na Soka, wengine waliotoweka katika kipindi hicho ni Jacob Mlay na Frank Mbise. Pamoja na kina Soka kutoweka Agosti mwaka jana, lakini Mei mwaka huu, mwanaharakati na mwanachama wa Chadema, Mdude Nyagali naye alitoweka baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana, nyumbani kwake Mbeya.
Ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, (LHRC) ya mwaka 2024 ilikusanya matukio 63 ya watu kupotea ama kutoweka katika mikoa ya Dar es Saaam, Kilimanjaro, Tanga na Arusha.
Agosti 22, 2024, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) ilieleza kuwa ilikuwa inafanya uchunguzi maalum kuhusiana na matukio hayo.
Mahakama yatupilia mbali ombi la CHADEMA, mashahidi kufichwa
DW imezungumza na viongozi wa Chadema, ambao wamesisitiza haki na nia ya dhati ya vyombo vya usalama kuhakikisha wanachama hao wanapatikana wakiwa hai. Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche amesema:
"Sio Soka tu, Kipanya, akina Mbise aliyekuwa na Soka, Ben Saa 8, wametekwa akina Azory Gwanda, ni mamia kwa mamia ya watu wametekwa mkiti wa vijana Wilaya ya Geita, hawa wote familia zao zinalia hazijui hatma yake, nini Chadema tunafanya kazi yetu ni kupiga kelele, na hatutawasahau."
Mnamo Juni 12 mwaka huu, akilivunja bunge la 12, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alitoa amri kwa vyombo vya usalama kufuatilia na kudhibiti matukio ya watu kutekwa na kutoeweka nchini mwake.