Mwadiplomasia wa juu wa EU: 'Hujuma zinaongezeka Ulaya'
1 Februari 2025Alipokuwa waziri mkuu wa Estonia, Kaja Kallas aliwakilisha watu milioni 1.3 katika taifa hilo dogo lilio katikati ya Urusi na Bahari ya Baltiki. Tangu alipochukua wadhifa wake kama mkuu wa masuala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwaka 2024, Kallas mwenye umri wa miaka 47 sasa anazungumza kwenye jukwaa la kimataifa kwa niaba ya watu takriban milioni 450 waliotapakaa katika nchi 27.
Lakini jambo moja halijabadilika: Kallas anaendelea kuelekeza umakini wake kwa Urusi.
"Ni wazi kwamba hujuma zinaongezeka barani Ulaya," Kallas alimuambia mwandishi wa DW Alexandra von Nahmen alipoulizwa kuhusu mfululizo wa mashambulizi yanayoshukiwa kuwa ya mchanganyiko, ya hivi karibuni yakiwa ni kebo za baharini katika eneo la kiuchumi la Sweden la Baltiki.
Soma pia: Waziri Mkuu wa Estonia asema hatonyamazishwa na Urusi
"Hatuwezi kweli kuona matukio haya kwa kujitenga, bali kama sehemu ya picha kubwa. Na kuelewa kwamba Urusi ina nia dhidi ya Ulaya na usanifu wa usalama wa Ulaya ambao haujabadilika," Kallas alisema katika mahojiano maalumu na DW kwenye makao makuu ya Huduma ya Mambo ya Nje ya Ulaya mjini Brussels siku ya Alhamisi.
Kama mtu alyezaliwa Estonia iliyokaliwa na Umoja wa Kisovieti, huenda si jambo la kushangaza kwamba Kallas ambaye ni mfuasi wa siasa za wastani, amejijengea jina kama mmoja wa wakosoaji wakali wa Moscow na waungaji mkono kinda wa Ukraine.
Marekani, EU 'bado marafiki,' Kallas asema
Kwa sasa, hiyo inamaanisha kufanya kazi kwa karibu na utawala mpya wa Rais wa Marekani Donald Trump, ambao umejaa wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia.
Pamoja, Marekani na nchi za EU zimetoa silaha na msaada kwa Ukraine kwa miaka mitatu. Lakini katika wiki chache za kwanza za utawala wake, Trump hakupoteza muda kuikosoa EU kuhusu biashara na matumizi ya ulinzi. Pia aliishtua Ulaya kwa kutangaza azma yake ya kuchukua udhibiti wa eneo huru la Denmark, Greenland.
"Bado sisi ni marafiki. Bado ni washirika," Kallas alisema kuhusu uhusiano wa EU na Marekani. "Wao ni washirika wetu wakubwa kwa upande wa uchumi, lakini pia kwa upande wa usalama."
"Niliweza kufanya mazungumzo mazuri sana na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio wiki hii. Tulikuwa tukijadili maeneo mbalimbali duniani ambapo tunashirikiana na pia kuona maeneo ambapo tunaweza kufanya zaidi," alisema. "Hivyo, mimi ni mwenye matumaini kuwa tuna uhusiano mzuri."
Na kuhusu Greenland?
"Ni wazi kwamba Marekani ni sehemu ya makubaliano ya kimataifa. Makubaliano ya kimataifa yanayosema kwamba lazima unapaswa kuheshimu uhuru wa maeneo […] na sina shaka kwamba wataheshimu hivyo," Kallas alisema.
Alipoulizwa ikiwa EU inaweza kufikiria kuweka wanajeshi huko, Kallas alisema hakukuwa na majadiliano yoyote kuhusu suala hilo.
Picha sawa ya Ukraine, lakini mkakati hauko wazi
Kallas pia alionesha uelewa kuhusu mkakati wa Washington kuelekea Kyiv. "Wanaelewa kwamba ili kumaliza vita hii, tunapaswa kuweka shinikizo kwa Urusi, kwa sababu Urusi ndiyo ilianza vita hii."
Trump hapo awali alidai kuwa anaweza kufanikisha makubaliano ya amani kati ya Urusi na Ukraine ndani ya siku moja, na kuibua hofu kwamba anaweza kuishinikiza Kyiv kusaini makubaliano ya haraka ya amani juu ya kile ambacho EU ingeweza kuona kama masharti yasiyofaa ambayo yanaweza kuipa msukumo Moscow katika kampeni zaidi za kijeshi.
Soma pia: Mkuu wa sera za Kigeni ajae EU anamtazamo upi kuhusu Israel
Sasa akiwa madarakani, Trump anaonekana kuchukua msimamo mkali zaidi dhidi ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kuliko vile wengi walivyotarajia, ingawa pia amemkosoa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy.
"Rais Trump amekuwa na msimamo imara katika matamshi yake dhidi ya Putin," Kallas alisema. "Hivyo naona kwamba tunaona picha hii kwa njia inayofanana."
Lakini Rubio, mwenzake wa Marekani Kallas, alimwambia nini kuhusu mkakati wa Ukraine katika mazungumzo yao?
"Lazima pia tukutane ana kwa ana na kujadili mambo haya, lakini ni wazi kwamba wanataka kumaliza vita hii," alisema. "Kila mtu anataka kumaliza vita hii kwa sababu kila mtu anataka kuwepo amani. Lakini pia ni wazi, na hicho alichosema (Rubio), ni wazi kwamba amani lazima iwe endelevu."
Mabadiliko Marekani kama fursa kwa Ulaya?
Ulaya haiepuki kutetemeka kutokana na Trump, ambaye tayari amesitisha msaada wa kigeni wa Marekani na kuiondoa nchi yake katika makubaliano ya Tabianchi ya Paris. Lakini Kallas alijaribu kuonyesha kwamba kutokuwa na uthabiti kwa Marekani, pamoja na mabadiliko ya jumla katika hali ya kisiasa duniani, ni fursa kwa EU.
"Nadhani wakati huu tulionao sasa ni changamoto kubwa, lakini wakati huo huo, pia unatoa fursa kwa Umoja wa Ulaya kuwa mdau mkubwa wa kisiasa duniani."
"Utawala mpya wa Marekani […] unafanya nchi nyingine zote kuuangalia pia Umoja wa Ulaya kwa sababu sisi ni mshirika anayekubalika, sisi ni mshirika thabiti," Kallas alisema. "Hiyo pia inatupa fursa ya kukuza nguvu zetu za kisiasa."