Israel yashambulia Iran katikati ya tishio la Makombora
18 Juni 2025Mapema Jumatano, milipuko ilisikika mjini Tehran, kufuatia mashambulizi makali ya angani yanayofanywa na Israel, yakiulenga mji huo mkuu wa Iran.
Jeshi la Israel (IDF) lilitangaza kushambulia Tehran. Kwenye akaunti yake ya Telegram jeshi hilo limesema limeshambulia kituo cha urutubishaji urani na vituo vingine kadhaa vya kutengeneza silaha vinavyomilikiwa na utawala wa Iran.
Baadaye, IDF iliripoti kuwa imegundua makombora kutoka Iran yanayoelekea Israel tena, na kwamba Jeshi la Anga la Israel linafanya operesheni ya kuondoa tishio hilo.
Brigedia Jenerali Effie Defrin, msemaji wa jeshi la Israel amesema "tunalenga vituo vya kijeshi, wao wanashambulia nyumba za raia. IDF itaendelea kufanya operesheni kwa usahihi, kw anguvu na kwa uthabiti ili kuhakikisha usalama wa watu wa Israel."
Mapema, Jumatano, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Esmail Baghaei, akihojiwa na kituo cha televisheni ya Aljazeera, alitoa tahadhari kwamba uingiliaji wa Marekani katika mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya nchi yake, unaweza kuchochea ‘vita kamili'.
Iran yadai kudhibiti mifumo ya ulinzi wa angani ya Israel
Walinzi wa Mapinduzi wa Iran wamedai kufanya wimbi la 11 la makombora dhidi ya Israel. Wamesema mashambulizi hayo yanaashiria mwanzo wa mwisho wa mifumo ya ulinzi ya angani ya Israel.
Msemaji wa jeshi hilo Iman Tajik amesema Iran imetumia makombora ya Fattah aliyodai yalishinda mifumo ya ulinzi ya Israel, na kutaja tukio hilo kuwa ujumbe kwa Marekani.
"Usiku wa leo, makombora yenye nguvu na uwezo wa kujigeuza ya Fattah yalitikisa mara kwa mara makazi ya Wazayuni waoga baada ya kupenya ngao yao ya ulinzi wa makombora, yakifikisha ujumbe wa nguvu wa Iran kwa mshirika wa Tel Aviv anayependa vita, aliyepotea katika ndoto na fikra zisizo na msingi."
Mzozo huo unaotishia kutanuka, umetia wengi wasiwasi na baadhi ya mataifa yakianza kuchukua hatua za tahadhari.
Ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem umechapisha kwenye tovuti yake kwamba ubalozi huo utafungwa hadi Ijumaa. Taarifa hiyo pia imewaagiza wafanyakazi wa serikali kuchukua tahadhari. Ubalozi huo umesema kuwa kufungwa huko ni "kutokana na hali ya sasa ya usalama na mzozo unaoendelea kati ya Israel na Iran."
Israel, China na Ugiriki zawarudisha nyumbani raia walioko nje
Mapema siku ya Jumatano, ndege mbili kutoka Cyprus zilitua mjini Tel Aviv. Kulingana na msemaji wa uwanja wa ndege wa Ben Gurion, Lisa Dvir, ndege hizo zilikuwa za kwanza za uokoaji kuwarejesha Waisraeli walioko nje ya nchi tangu mzozo wao na Iran ulipogeuka zogo.
China kupitia wizara yake ya Mambo ya Nje imesema takriban raia wake 800, wameondolewa Iran tangu Israel ilipoanza mashambulizi ya angani dhidi ya Iran wiki iliyopita.
Rais wa China Xi Jinping ametoa wito wa kupunguza mvutano huo haraka iwezekanavyo. Xi amesema kuwa China "ina wasiwasi mkubwa kwani operesheni ya kijeshi ya Israel dhidi ya Iran imesababisha ongezeko la ghafla la mvutano katika Mashariki ya Kati. Alisema hayo Jumanne akiwa Kazakh, mji mkuu wa Astana.
Kulingana na mashirika ya kutetea haki za binadamu, tangu mzozo huo uanze wiki iliyopita, watu wasiopungua 585 wameshauawa kote nchini Iran na 1, 326 kujeruhiwa
Nchini Israel, watu 24 wameuawa, kufuatia mashambulizi ya Iran ya kulipiza kisasi. Inakadiriwa kwamba hadi sasa Iran imefyatua makombora 400 na mamia ya droni dhidi ya Israel.
AP, APTN, RTRE