Mvutano waibuka kuhusu uteuzi wa makamishna wa IEBC Kenya
12 Mei 2025Muungano wa upinzani nchini Kenya umemshutumu Rais William Ruto kwa kuwateua makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) bila mashauriano ya pamoja, hatua wanayosema inaweza kuhatarisha uhalali wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, amesema uteuzi huo umepuuzilia mbali mapendekezo ya mazungumzo ya kitaifa yaliyoainishwa kwenye ripoti ya NADCO, akisisitiza kuwa uteuzi wa Erastus Edung Ethekon kuwa mwenyekiti mpya wa IEBC ni ukiukaji wa uwiano wa kisiasa na kunapunguza imani ya umma kwa tume hiyo.
"Huwezi kuwa mchezaji na refarii halafu uchague refarii wako. Haiwezekani," alisema Kalonzo wakati wa mazishi katika eneo bunge la Matungulu, Kaunti ya Machakos.
Kauli kama hiyo imetolewa na Kiongozi wa chama cha DAP-K, Eugene Wamalwa, aliyesema kuwa serikali imevunja misingi ya mashauriano ya Bomas kwa kutotekeleza makubaliano ya pamoja.
"Mmekiuka maelewano ya Bomas. Mmekataa mashauriano. Lakini bado tuko tayari kwa chochote!"
Upinzani kuwasilisha kesi mahakamani
Wabunge kutoka jamii ya Wakamba, akiwemo Mbunge wa Kathiani, Robert Mbui, na Seneta wa Makueni, Daniel Maanzo, wametangaza kuwa upinzani utawasilisha kesi mahakamani kupinga uteuzi huo wakitaja upendeleo na uhusiano wa kifamilia kuwa vigezo vilivyotumika.
"Huu ni upendeleo wa wazi. Tutaenda mahakamani," alisema Maanzo.
Soma pia: Rais Ruto aidhinisha marekebisho Tume ya Uchaguzi IEBC
Kwa upande wao, viongozi wa muungano wa Kenya Kwanza wakiongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang'ula, wamewataka wanasiasa wa upinzani kufuata taratibu za kisheria iwapo wana pingamizi kuhusu uteuzi huo.
"Mwananchi anayepinga peleka malalamiko yako kwa Kamati ya Sheria na Haki ya Bunge la Kitaifa, maarufu kama JLAC," alisisitiza Wetang'ula.
Rais Ruto alimteua Erastus Edung Ethekon – mwanasheria kwa taaluma – kuwa Mwenyekiti mpya wa IEBC siku ya Alhamisi. Sambamba na hilo, aliwateua makamishna saba wapya: Anne Njeri Nderitu, Moses Alutalala Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor Hassan, Francis Odhiambo Oduol, na Fahima Araphat Abdallah. Majina yao yamewasilishwa kwa Bunge la Kitaifa kwa ajili ya kuidhinishwa kulingana na sheria za IEBC.
Viongozi wa Kenya Kwanza wameunga mkono kikamilifu uteuzi huo, wakisema ni hatua muhimu kuelekea kuanzishwa kwa mchakato wa kura ya maoni kuhusu marekebisho ya katiba na upangaji wa mipaka ya maeneo ya uchaguzi, kama ilivyopendekezwa katika ripoti ya Kamati ya Majadiliano ya Kitaifa.