Mvua zasimamisha shughuli za uokozi Pakistan
18 Agosti 2025Mvua hiyo kubwa iliyonyesha kote nchini humo tangu Alhamisi iliyopita imesababisha mafuriko, kuongezeka kwa kina cha maji na maporomoko ya ardhi yaliyozingira vijiji kadhaa na kuwaacha mamia wakiwa wamekwama kwenye vifusi.
Zaidi ya watu 320 waliripotiwa kufa kaskazinimagharini mwa jimbo la Khyber Pakhtunkhwa, hii ikiwa ni kulingana na idara ya masuala ya dharura ya jimbo hilo ambayo pia imeonya juu ya mafuriko mengine hadi siku ya Alhamisi.
Watoa misaada wa kujitolea wamekuwa wakiwahimiza mamia ya waokozi kufanya kila linalowezekana kuwapata manusura na kuinasua miili iliyokwama katikati ya hofu hiyo ya mvua nyingine kubwa ambayo tayari imeanza jimboni humo.
Miili mingi bado imekwama chini ya vifusi
"Asubuhi ya leo mvua nyingine imeanza kunyesha na kusababisha operesheni za uokozi kusimama," alisema Nisar Ahmad, 31, anayejitolea kwenye operesheni hizo katika wilaya iliyoathirika sana ya Buner, ambako "vijiji 12 vilifunikwa kabisa huku miili 219 ya watu ikinasuliwa kwenye vifusi vya matope."
"Miili mingi bado imefukiwa kwenye vifusi vya matope na mawe, na inaweza kunasuliwa kwa kutumia mashine nzito tu" aliongeza.
Karibu watu 200 bado hawajulikani walipo kwenye jimbo la Khyber Pakhtunkhwa, zimesema mamlaka za eneo hilo.
Watu wengi wamekimbia ili kujitafutia hifadhi chini ya miundombinu iliyoharibiwa na kwenye maeneo na milimani kwenye kijiji hicho cha Burner, ambalo lina miinuko mikali.
"Hata kama kukinyesha mvua kidogo hivi sasa, tunaogopa kwa sababu hata kulipotokea mafuriko, hakukunyesha mvua kubwa. Lakini watu ambao hatakutarajiwa, walisombwa na na dhoruba," alisema mkazi wa Buner Hussain, 35.
"Watoto na wanawake wanakimbilia milimani wakipiga mayowe ya kuomba msaada," alisema Hazrat Ullah, 18, alipozungumza na AFP.
Mtoa huduma za dharura anayejitolea, Ahmad amesema pia kuna wasiwasi wa upatikanaji wa chakula na maji safi huko siku ya usoni.
Mabaki ya mifugo yasababisha harufu kali nchini humo
"Mifugo mingi imekufa kutokana na mafuriko na miili yao inayooza inatoa harufu mbaya inayosambaa kwenye maeneo mengi. Hivi sasa, tunachohitaji kwa haraka ni maji ya kunywa, na ninatoa wito kwa serikali kutuletea" alisema.
Mvua kubwa za karibu robo tatu ya mvua za mwaka mzima kwenye ukanda wa Asia Kusini hunyesha katika majira ya mvua kubwa za "monsoon", na hutumiwa kwa shughuli za kilimo na kwa upande mwingine husababisha uharibifu mkubwa.
Kulingana na Shirika la Kitaifa la Maafa, nguvu ya monsoon za mwaka huu ni karibu asilimia 50 hadi 60 kuliko mwaka jana.
Maporomoko ya ardhi na mafuriko ya ghafla ni ya kawaida wakati wa msimu wa upepo mkali na mvua, ambao kwa kawaida huanza Juni hadi mwishoni mwa Septemba.