Mvua yasababisha vifo na maafa Kongo
7 Aprili 2025Idadi hiyo ya waliofariki dunia pamoja na majeruhi kama ilivyotangazwa na waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu ya DRC Jacquemain Shabani, huenda ikaongezeka zaidi kwani, bado juhudi za kuwatafuta watu zinaendelea, na huenda kuna watu waliokwama kwenye nyumba zilizozama.
Serikali ya Congo imetayarisha nafasi mbalimbali, kwa ajili ya kuwahifadhi mamia ya raia ambao nyumba zao zimezama na wengine ambao nyumba zao zimeporomoka kutokana na maporomoko ya ardhi, kama anavyosema hapa waziri wa mambo ya ndani Jacquemain Shabani, akitupatia matokeo ya awali ya mafuriko.
Soma pia:Mvua kubwa yauwa zaidi ya watu 30 Kinshasa
"Tumeshudia athari nyingi kwenye barabara nambari moja. Na pia miporomoko ya ardhi ambayo ilichukuwa nyumba kadhaa na iliyosababisha vifo vya watu pamoja na majeruhi wengi." Alisema Waziri wa Mambo ya Ndani.
Aliongeza kwamba tathmini iliyofanyika hapo jana ilionesha kuwa watu ishirini na wawili waliuwawa na majeruhi arobaini na sita walijeruhiwa kufuatia mvua hizo na sasa wanapatiwa matibabu na wengine wanahifadhiwa kwenye kituo kimoja huko Kimwenza.
Miundombinu yaathirika vibaya
Na ilikuhakikisha kwamba barabara ya kwenda uwanja wa ndege wa mjini Kinshasa, Ndjili, ukarabati wa haraka unafanyika, ili kuwarahisishia wasafiri waweze kuwasili mapema kwenye uwanja huo wa ndege, kamishna wa polisi mjini Kinshasa Claude Kilimbalimba,anaelezea.
"Tumekuwa tukiondoa magari yote yaliyokwama kati ya daraja Matete na daraja Ndjili na zile zilizoko kati ya daraja Ndjili na Apocalypse."
Alisema afisa huyo wa polisi na kuongeza kwamba maeneo yote hayo yanapashwa kubaki wazi ilikurahisishia kazi mafundi wanaotengeneza daraja.
"Kuna pia mbali na daraja, nyumba kati ya miatano na mia sita zimezama kwenye Abatoir petro Congo. Kuna boti pamoja na mitumbwi iliyowekwa tayari kwaajili ya kuwaokoa raia na kuwapeleka kwenye maeneo yaliyo salama."
Soma pia:Kongo yaandaa mkutano wa kilele wa kuiboresha misitu barani Afrika
Baadhi ya wasafiri ambao wamepata adha ya usafiri wanasema kumekuwa na ongezeko la nauli, lakini pia kumeshuhudiwa uhaba wa usafiri kutokana na miundombinu ya kawaida ikiwemo barabara kuharibika.
"Tumekuja hapa kwa boti kutoka Beach hadi hapa Kinkole. Watu unaowaona hapa wanasafiri na barabara ya Ndjili haipitiki. Dola miamoja na hamsini ndio nimelipa kama nauli kutoka Beach Ngobila hadi Kinkole. Kuna wale waliolipa dola miambili za kimarekani ili kwenda uwanja wa ndege."
Juhudi za kuwatafuta watu zikiwa bado zinaendelea, utabiri wa hali ya hewa umebaini, kuwa mvua nyingi zitanyesha mjini Kinshasa, na watu wanaoishi kwenye maeneo ya hatari, wametakiwa kuchukua hatua, za kuyahama maeneo hayo.
Wataalamu wa masuala ya ujenzi wamesisitiza kwamba, ujenzi wa magorofa na nyumba nyingi hapa jijini Kinshasa, unafanywa bila ya kuheshimu kanuni na ndio sababu ya kutokea majanga kama haya.