Mvua kubwa yasababisha maafa makubwa Rwanda
19 Agosti 2025Wizara inayoshughulikia majanga nchini Rwanda imesema kwamba watu wanne kati ya waathirika hao wamekufa kutokana na kupigwa na radi katika majimbo ya mahgharibi na kaskazini mwa nchi huku mtu mwingine akiangukiwa na kifusi baada ya nyumba alimoishi kukumbwa na maji kadhalika katika jimbo la kaskazini mwa nchi.
Tangu siku ya jumapili usiku hadi jana jioni katika sehemu zote za nchi imekuwa ikinyesha mvua kali ambayo hata hivyo haikutegemewa kwa sababu siku zote mwezi wa nane unakuwa ni kiangazi nchini Rwanda
Idadi ya waliokufa kwa mafuriko Rwanda yafikia 130
Katibu mkuu katika wizara ya kudhibiti na kukabiliana na majanga nchini Rwanda Ngoga Aristarque amesema kwamba haikutegemewa kupata mkasa huu ambao umegharimu hata maisha ya watu
"Kwa kawaida mwezi wa nane unakuwa ni mwezi ambao daima hauna mvua ya aina yoyote, lakini ninaweza kusema kwamba ni mabadiliko ya hali ya hewa ambayo lakini yamesababisha hasara maana tangu tarehe kumi na sita tumekuwa na mvua kali ambayo imesababisha maisha ya watu 5 kupotea na wengine kujeruhiwa.”
Mamlaka ya hali ya hewa imetoa angalizo kwa wananchi kuwa makini kutokana na hali ya hewa kuendelea kubadilika hali ambayo huenda ikasababisha kunyesha kwa mvua kali msimu huu. Mamlaka hiyo imesema kwamba hata leo siku ya jumanne Rwanda inategemea kupata mvua nyingi ingawa hadi sasa haijanyesha isipokuwa hali ya kibaridi na wingu zito linaloonekana kutanda katika maeneo mengi.
Watu 109 wafariki kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa Rwanda
Alicia Kairangwa ni mkazi wa Kigali yeye kama walivyo wengi ana maoni kuhusu mvua hizi zilizonyesha katika wakati ambao haukutegemewa
Wasiwasi kwa baadhi ya wananchi ni kwamba ikiwa mvua hizi zinasababisha vifo wakati huu wa kiangazi itakuwaje yatakapoanza masika? Rwanda ni nchi yenye milima na miinuko mikali na kila mara mvua zinaponyesha mali na baadhi ya watu husombwa na maji kutokana na mafuriko na kuangukiwa na vifusi.
Serikali hata hivyo hadi sasa imeendelea na kampeni ya kuwahamisha wananchi kutoka maeneo hatarishi lakini bado hatua hii haijazuia kuwepo kwa hasara kubwa kila mara mvua za aina hii zinaponyesha.