MUZAFFARABAD: Wanajeshi wa Pakistan waanza kuusafisha mji wa Muzaffarabad
24 Oktoba 2005Jeshi la Pakistan limesema limeanza kulisafisha eneo la soko kubwa la Medina katika mji mkuu wa eneo lake la Kashmir, Muzaffarabad, ambako maiti nyingi bado zimezagaa majuma mawili tangu tetemeko la ardhi kutokea nchini humo.
Msemaji wa jeshi, meja Farooq Nasir, amesema eneo hilo halingeweza kufikiwa kufuatia uharibifu mkubwa uliosababishwa na tetemeko hilo. Wafanyikazi wa mashirika ya misaada wamezitoa maiti katika vifusi, huku umoja wa mataifa ukionya kwamba watu takriban elfu 800 bado hawana mahema.
Huku misaada ikiendelea kuongezeka polepole, vikosi vya wanajeshi na watoa misaada wa mashirika ya kigeni wameanza kupeleka misaada katika vijiji na maeneo ya milimani, ambako maelfu ya watu wanahitaji misaada kwa dharura.
Msichana wa miaka 12 amefariki dunia leo wakati hema lao lilipowaka moto katika mji wa kazkazini wa Balakot. Msichana huyo pamoja na kijana, ambao jamaa zao waliangamia kufuatia tetemeko la ardhi, walichomeka vibaya na kupelekwa hospitali, lakini akafariki dunia kwa majeruhi aliyoyapata. Maisha ya kijana huyo wa miaka 7 yamo hatarini.