Muyaya: Congo yaikabili Rwanda pande zote
8 Machi 2025Katika mahojiano maalumu ya DW, Muyaya, ambaye pia ni waziri wa mawasiliano na habari wa Congoameituhumu Rwanda kwa kuhusika moja kwa moja na mgogoro unaoendelea mashariki mwa Congo, akisema wanaendelea kuzishambulia kwa mabomu kambi za wakimbizi, hospitali, kuua watu wasio na hatia na wasanii.
Akizungumzia uwezo dhaifu wa jeshi la Congo kiasi cha kushindwa kuepusha miji kuanguka mikononi mwa waasi, Muyaya ameieleza hali kuwa tete. Aliongeza kusema kwamba rais wa Rwanda Paul Kagame aliamua kupigana vita nchini Congo kwa sababu ya mageuzi yanayoendelea Congo na mafanikio yaliyopatikana.
Muyaya alisema haiwezekani kuyasuluhisha matatizo yanayolikabili jeshi la Congo wala kukamilisha mageuzi katika jeshi katika kipindi cha miaka mitano ya awamu ya utawala wa rais, lakini Congo itaelekeza nguvu zaidi na kuendelea na mchakato wake wa mageuzi kuhakikisha jeshi linakuwa imara na nguvu.
"Hali ni ngumu, hasa unapolizungumzia jeshi la Congo. Usisahau kwamba hali hii ilianzia baada ya kuanguka kwa Mobutu, kulikoongozwa na Kaberebe, ambaye ni mwanajeshi wa Rwanda aliye chini ya vikwazo vya Marekani. Halafu kukaja makubaliano ya Sun City kati ya vyama na makundi mbalimbali. Tukavichanganya pamoja vikosi vyote vya kijeshi kutokea Rwanda hasa RCD na MLC kutoka kwa jeshi la kawaida la wakati wa utawala wa Kabila. Unapoyachanganya hayo yote, unapata kitu ambacho sio rahisi kukielezea kama jeshi imara lenye uwezo wa kupigana kwa pamoja."
Muyaya pia aliituhumu Rwanda kwa kuwa nchi ya uongo, akisema ni wazi kwamba rais Kagame anafahamu vyema zaidi kuliko mtu yoyote kwamba wanajeshi wako katika ardhi ya Congo na baadhi yao wanakufa huko. Muyaya alikumbusha kuhusu mahojiano aliyofanyiwa Kagame na kituo chao ha televisheni cha CNN na alipoulizwa kama wanajeshi wake wako nchini Congo alisema hafahamu.
Mkataba wa madini na Marekani
Kuhusu uwezekano wa mkataba wa madini kati ya Marekani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Muyaya alisema lengo la kwanza ni kutanua wigo wa wawashirika wao. Kama miongoni mwa washirika hao ni Wamarekani, anadhani hilo lilikuwa lengo kuu la rais Tshisekedi. Muyaya alisema wapo pia Wachina, Wajapani na nchi nyingine kama vile India na Uswisi.
Muyaya aliongeza kusema madini ya Congo yanaibiwa na wamekuwa wakifanya juhudi kuzuia wizi huo kuhahakisha madini yanauzwa kwa njia ya haki, lakini vita vinavyoendelea vilianzishwa kwa lengo la kuvuruga mchakato mzima wa mageuzi na kukwamisha juhudi za kuidhubiti sekta ya madini ya Congo.
"Kama kutakuwa na masilahi yoyote, bila shaka, kutafanyika mazungumzo. Lakini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo inahitaji usalama na kama usalama huu unaweza kutoka kwa baadhi ya ushirikiano wetu na Marekani, basi si vibaya."
Suala la msaada wa maendeleo
Kuhusu suala la msaada, Uingereza, Canada na Ujerumani kwa mfano tayari zimesitisha msaada wa maendeleo. Umoja wa Ulaya ungali bado unatia na kutoa kuhusu kuchukua hatua kali. Alipoulizwa, Congo watarajie nini kutoka kwa viongozi wa Ulaya, Muyaya alisema wanatarajia wachukue hatua kulingana jinsi wanavyotakiwa kufanya.
"Tumeona mfano wa uvamizi barani Ulaya na tuliona jinsi nchi nyingine za Ulaya zilivyochukua hatua kujivu uchokozi huo. Tunajiuliza maswali kama hayo, kwa nini hawachukui hatua kama walivyofanya barani Ulaya? Hatua ya kwanza ya vikwazo bila shaka tunaifurahia, lakini tunafahamu haitoshi. Hata rais Kagame wakati alipoelezea kwa nini anaishambulia Congo alisema vikwazo havitamzuia kufanya anachokifanya. Ni wazi kwamba haheshimu wala kuzingatia sheria ya kimataifa na Umoja wa Ulaya hauwezi kuvumilia tabia hii." Akasema Muyaya.
Soma pia: Ujerumani yasitisha msaada mpya kwa Rwanda
"Ndio maana wanatakiwa wachukue hatua haraka wahakikishe watakapofanya hivyo, rais Kagame anawaondoa haraka wanajeshi wake nchini mwetu Congo kwa sababu si mahali wanapotakiwa kuwepo. Hili lazima liwe wazi. Tunafurahi kuona hatua imeanza kuchukuliwa. Tunataka kuona hatua hizi zinakuwa imara zaidi ili Kagame aliondoe jeshi lake nchini mwetu." Aliongeza kusema.